Beki, kocha wazua mzozo

Muktasari:

Hali hiyo imetokea baada ya Spurs kukubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Arsenal

London, England. Beki kisiki wa Tottenham Hotspurs, Danny Rose, ameibua mzozo na kocha wake Mauricio Pochettino.

Beki huyo wa kushoto ameibua mzozo huo baada ya kupumzishwa katika mchezo ambao Spurs ilichapwa mabao 2-0 na Arsenal.

Rose alifanya mazoezi Jumamosi asubuhi akionekana yuko fiti asilimia 100, lakini Pochettino alimtoa.

Baada ya kutolewa, Rose alionyesha hasira kwa bosi wake alipokuwa  akielekea kwenye benchi.

Beki huyo anahusishwa na mpango wa kujiunga na Man United katika usajili wa dirisha dogo Januari, mwakani.

Rose alirejea uwanjani kwa mara ya kwanza akitokea katika maumivu ya mguu yaliyomuweka nje ya uwanja muda mrefu kabla ya kuivaa Arsenal.

Mchezaji huyo mwenye miaka 27, alitaka kucheza dakika 90 ili kupata nafasi ya kuitwa katika timu ya taifa ya England kwa fainali za Kombe la Dunia.

Kocha huyo alitetea uamuzi akidai  Rose alikuwa nje ya uwanja miezi 10, hivyo hakuwa fiti kucheza dakika 90.