Batambuze: Narudi Singida

Muktasari:

Singida imeweka kambi jijini Mwanza lakini mchezaji huyo ni miongoni mwa wachezaji ambao hawajajiunga na timu hiyo huku ikisemekana kuna mgomo baridi kutokana na madai yao.

BEKI kisiki wa Singida United, Shafik Batambuze, ambaye ni raia wa Uganda bado hajajiunga na kikosi hicho katika maandalizi ya msimu ujao, lakini amewaambia mabosi na mashabiki wake wasiwe na wasiwasi.

Singida imeweka kambi jijini Mwanza lakini mchezaji huyo ni miongoni mwa wachezaji ambao hawajajiunga na timu hiyo huku ikisemekana kuna mgomo baridi kutokana na madai yao.

Lakini akizungumza na Mwanaspoti, Mganda huyo alikiri hajajiunga na wenzake katika maandalizi hayo, lakini alisema anatarajia kurejea hivi karibuni.

“Mimi bado nipo Singida na ni mchezaji wao, kuna mambo madogo madogo ninayoyaweka sawa huku kisha nakuja,” alisema.

Akizungumza kuhusu kukaa bila kufanya mazoezi na timu yake, alisema alikuwa akijifua na timu ya taifa ya kwao, The Cranes.

“Nipo na timu ya Taifa na hivi karibuni tulicheza mechi ya kirafiki, si unajua timu inajiandaa kucheza na Tanzania, lakini bado haijakamilika,” alisema.