Baobao Queens yaota nne bora

Muktasari:

Timu hiyo inashiriki Ligi Kuu ya Wanawake inayofanyika kwa mara ya kwanza Tanzania Bara

Dodoma. Wakati Ligi Kuu ya soka la wanawake ikitarajiwa kuanza kutimua vumbi lake Novemba 26 katika vituo vya Dar es Salaam na Arusha, kocha Baobab Queens ya Dodoma, Mussa Furutuni ametamba kikosi chake kipo tayari kusaka ubingwa huo.

Kocha huyo alisema maandalizi waliyoyafanya kwa zaidi ya miezi mitatu yanatosha kabisa kwa timu yake kufanya vema kwenye ligi hiyo na anaamini timu yake itakuwa kati ya timu 4 zitakazotinga raundi ya pili.

“Kiukweli maandalizi ya timu yangu safari hii ni tofauti na msimu uliopita kwani nimepata muda mzuri wa kuiandaa timu hii kuelekea kwenye ligi ijayo ya kituo na bila shaka ni imani yangu timu yangu ni mojawapo ya timu 4 zitakazofuzu raundi ya pili baada ya kituoni”.alisema Furutuni

 

Timu hiyo ya Baobab imepangwa kituo cha Arusha pamoja na Alliance Academy na Marsh Academy zote za Mwanza, Majengo Sisters ya Singida, Panama Queens ya Iringa na Kigoma Sisters ya Kigoma.

 

Kituo cha Dar es Salaam kina timu za Simba Queens, Mburahati Queens, JKT Queens, Evergreen Queens zote za Dar es Salaam, Fair Play ya Tanga pamoja na bingwa mtetezi Mlandizi Queens.