Azam waukamia ubingwa Bara

Muktasari:

  • Pluijm alisema kwa aina ya wachezaji alionao na uchu walionao wa kutaka kubeba taji kwa mara nyingine, anaamini jambo hilo litawezekana mwishoni mwa msimu.

AZAM FC imewahi kubeba mara moja tu taji la Ligi Kuu Bara msimu wa 2013-2014, lakini sasa unaambiwa Kocha Mkuu wake, Hans Pluijm amesema wanalitaka taji hilo tena na haoni sababu ya kuwazuia wasilibebe, licha ya ushindani uliopo msimu huu.

Pluijm alisema kwa aina ya wachezaji alionao na uchu walionao wa kutaka kubeba taji kwa mara nyingine, anaamini jambo hilo litawezekana mwishoni mwa msimu.

Kocha huyo wa zamani wa Yanga na Singida United, alisema kitendo cha kutoa nyota kadhaa kujiunga na timu za taifa mbalimbali ni faida kwao ndio maana anaamini taji la Ligi Kuu linawahusu.

Alisema katika kujiweka sawa ndio maana walikuwa wakiendelea kujifua kwa mechi kadhaa za kirafiki ambapo amebaini makosa katika safu yake ya ulinzi na sasa anafanyia kazi ili kila kitu kiende sawa.

“Tumecheza michezo mitatu ya kirafiki tukifunga mabao manne na kuruhusu matatu ikiwa na maana kuna umakini mdogo kwa mabeki wangu tatizo nililoanza kulifanyia kazi na kubwa nililoliona ni upana wa kikosi kilicho na uchu wa mafanikio,” alisema.