Azam Tv kulipia mashabiki 250 kuziona Simba, Yanga

Muktasari:

  • Uwanja wa Taifa una uwezo wa kuchukua mashabiki 60,000 kwa wakati mmoja

Dar es Salaam. Kampuni ya Azam Tv yenye haki za kurusha matangazo ya Ligi Kuu Bara, imeweka wazi kuwa italipia wateja wao 250 kuangalia pambano la Simba dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Taifa Septemba 30.

Afisa Masoko wa Azam Tv, Abdul Mohammed, aliwasisitiza wateja wao kulipia ving'amuzi vyao kwani ndio watapata fursa hiyo ya kujipatia tiketi ya kuona mechi ya Simba dhidi ya Yanga.

"Tiketi watapata wale ambao watalipia ving'amuzi vyetu kwa shilingi elfu ishirini na nane na ndio wataingia katika kupata tiketi za kukaa katika VIP uwanja wa Taifa."

Abdul alifunguka zaidi kuwa watahakikisha watazamaji wao wanapata picha nzuri kupitia ving'amuzi vyao wakiwa nyumbani wakiangalia vipindi vya michezo na vipindi vingine.

"Ving'amuzi ambavyo ni vibovu tutavipokea na kuwapa vipya, lakini wanatakiwa walipie miezi minne na ndio watapata fursa ya kupewa ving'amuzi vyetu vipya bure," alisema Abdul.