Azam FC yakaa kileleni kwa muda

Muktasari:

Azam imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara mmoja tangu wakati huo imeshindwa kurudia rekodi hiyo.

Dar es Salaam. Azam FC itaongoza Ligi Kuu Bara kwa muda baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Mwadui FC katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Mwadui Complex.

Azam inakaa kileleni ikiwa na pointi saba sawa na Mbao FC kwa kuwa na idadi kubwa ya mabao, baada ya Coastal Union kulazimishwa suluhu African Lyon.

Matokeo hayo yanaifanya Coastal Union kufikisha pointi sita hivyo Azam kubaki kileleni mpaka kesho Jumamosi kusubiri matokeo ya Simba na Ndanda FC.

Katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa, Azam ilikuwa wa kwanza kupachika bao dakika ya 55, kupitia kwa Salum Aboubakary 'Sure Boy' aliyepiga shuti kali na kwenda moja kwa moja.

Bao la Mwadui la kusawazisha lilipachikwa dakika ya 71 na Edwin Innocent akitumia vizuri uzembe wa mabeki kushindwa kuokoa mpira uliopanguliwa na kipa wao.

Azam imetunza rekodi yake nzuri dhidi ya Mwadui katika michezo saba waliyokutana katika michezo wa Ligi Kuu Bara huku Azam ikishinda mara tano na sare mbili.

Kwenye Uwanja huo wa Mwadui Complex timu hizo zimekutana mara nne na Azam ikishinda mara mbili na kupata sare mbili.