Alliance Queens kupima mitambo yake Kenya

Muktasari:

  • Kocha wa Alliance, Ezekiel Chobanka alisema kabla ya kwenda Kenya kusaka mechi za kujipima ubavu, wataweka kambi jijini Dar es Salaam.

TIMU ya Alliance Queens ya jijini Mwanza inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) inatarajiwa kwenda Kenya kwa ajili ya mechi za kirafiki za kimataifa kujiweka sawa kwa ligi wanayoshiriki msimu huu.

Alliance itaenda nchi hiyo jirani Aprili 27 ikiwa ni kujiweka sawa kabla ya Ligi Kuu kuendelea tena baada ya kusimama kwa sasa kupisha mechi za kimataifa za timu ya taifa ya wanawake, Twinga Stars inayowania fainali za Afcon 2018.

Kocha wa Alliance, Ezekiel Chobanka alisema kabla ya kwenda Kenya kusaka mechi za kujipima ubavu, wataweka kambi jijini Dar kwa muda wa wiki moja na mazoezi watakuwa wanafanya Uwanja wa Karume.

"Tuna malengo ya kuchukua ubingwa na ndio maana hatuwezi kujibweteka kutokana na ligi kusimama, najaribu kuwaweka sawa wachezaji wangu."

"Natumia mapumziko kurekebisha mapungufu ambayo yamekuwa yakijitokeza hatua ya nane bora, naamini ligi ikianza tutakuwa na jipya. Tumemtuma mtu  Kenya, kuangalia ni timu gani tutakayocheza nao na sehemu ya kufikia pia," alisema.

Alliance ipo nafasi ya tatu ikiwa na alama saba tu baada ya kushuka uwanjani mara nne ikishinda mechi mbili, kupoteza moja na kutoka sare pia moja, huku vinawa wa ligi hiyo JKT Queens ikiwa kileleni na pointi 12 kisha Kigoma Sisters yenye alama 9.