Omog ajipanga kumlinda Ajibu

Muktasari:

  • Mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba amekuwa na mafanikio makubwa tangu alipotua Yanga msimu huu

Dar es Salaam. HABARI ya mjini wiki hii ni pambano la watani wa jadi Simba na Yanga ambalo litapigwa Jumamosi ya Oktoba 28, kwenye uwanja wa Uhuru.

Kocha wa Simba, Mcameroon Joseph Omog amewaambia wachezaji wake kwamba wakiweza kudhibiti ubora na akili za miguu ya Ibrahim Ajibu na Obrey Chirwa kazi imeisha.

“Nimewaangalia Yanga, wana timu nzuri Ajibu na Chirwa ni miongoni mwa wachezaji hatari kwa sasa katika kikosi hicho na katika mechi yetu nitahakikisha hawapati nafasi ya kupewa pasi za hatari ambazo zitakuwa na madhara langoni kwetu,”alisema kocha huyo ambaye mashabiki wa Simba wanahisi Mrundi, Masud Djuma ameletwa kuchukua nafasi yake.

“Ajibu nilikuwa nae katika kikosi changu msimu uliopita na ana uwezo wa kukaa na mpira akapiga pasi ya mwisho ambayo itakuwa na madhara kwetu, lakini anaweza wa kufunga muda wowote kama atapata nafasi.

“Chirwa ana uwezo wa kukaa na mpira na ana uwezo wa kukimbia huku akiwa na mpira mguuni na anaweza kufunga pia, nimeliona hilo na nitakaa na wachezaji wangu ili kuhakikisha hawapati nafasi kama hizo,” alisema.

“Katika kambi yetu ya wiki moja huko Zanzibar miongoni mwa mazoezi ambayo tutakuwa tunafanya ni kupunguza makosa ambayo yamejitokeza katika mechi zetu zilizopita haswa katika safu ya ulinzi ambayo ndio itakuwa na kazi ya kuzuia washambuliaji wa Yanga,” alisema Omog.