Acheni kutupania Kagera Sugar jamani!

Muktasari:

"Kuna msemo unasema  sifa yako ndiyo jaribu lako, Kagera kwa sasa inatupiwa jicho tofauti na jinsi ilivyokuwa awali, hii ni kwa sababu ya kumaliza nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi mwaka jana, tutaendelea kukomaa ili kuwathibitishia wadau kwamba hatukubahatisha," anasema.

KIUNGO mkongwe wa Kagera Sugar, George Kavila amesema kumaliza nafasi ya tatu msimu ulioisha ni kama wamejipalia mkaa kichwani wa kukamiwa na wapinzani wao katika ligi inayoendelea.
"Kuna msemo unasema  sifa yako ndiyo jaribu lako, Kagera kwa sasa inatupiwa jicho tofauti na jinsi ilivyokuwa awali, hii ni kwa sababu ya kumaliza nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi mwaka jana, tutaendelea kukomaa ili kuwathibitishia wadau kwamba hatukubahatisha," anasema.
Kavila anasema ugumu wanaokumbana nao utawaongezea ubora zaidi na kuhakikisha msimu huu wanaongeza juhudi na viwango vyao kuwa juu.
"Hii inatufumbua macho kuona kila hatua tunatakiwa kupambana na siyo kuridhika na mafanikio ya mwaka jana, tunajiamini haijalishi tutakutana na ushindani wa kiasi gani, lazima tuwe na mtazamo hata wa kutoka wachezaji bora, wafungaji bora," anasema.
Ameuzungumzia uzoefu wake katika ligi kwamba, unamsaidia kujua zaidi soka linahitaji nini na kupelekea kudumu kwenye kiwango na kuwapiku baadhi ya chipukizi wanaopanda na kushuka uwezo wao.
"Kadri siku zinavyokwenda ndivyo unavyozidi kuwa bora, lakini inatokana na kuuheshimu mpira, hii inapaswa kuigwa na chipukizi kujitunza na kujua soka linahitaji nini vinginevyo watakuwa wanachungulia kwenye ligi na kuondoka," anasema.