Ukuta wa Man United majanga

Muktasari:

Lakini, mabao matatu ya kipindi cha kwanza ambayo safu yake ya ulinzi ikiongozwa na Eric Bailly na Victor Lindelof imerushu, yametosha kufichua siri nzima kuhusiana na kikosi cha Manchester United.

WAKATI kocha Jose Mourinho akipambana kusaka beki wa maana kwa ajili ya kuimarisha kikosi chake wengi hawakumulewa.
Lakini, mabao matatu ya kipindi cha kwanza ambayo safu yake ya ulinzi ikiongozwa na Eric Bailly na Victor Lindelof imerushu, yametosha kufichua siri nzima kuhusiana na kikosi cha Manchester United.
Mourinho na jeshi lake lilisafiri hadi Uwanja wa Amex kuikabili Brighton na kama kawaida ikakutana na kipigo cha mabao 3-1. Mabao yote yalifungwa kwenye kipindi cha kwanza na jitihada za United kurudisha zilikwama licha ya kupiga mpira mwingi.
Kipigo hicho kimeifanya Man United kuwa wanyonge wa Brighton, ambapo rekodi zinaonyesha kuwa haijawahi kushinda kwenye Uwanja wa Amex, ambapo msimu uliopita pia walichapwa.
Katika mchezo huo, Man United walionekana hovyo kwenye kipindi cha kwanza na kuwapa Brighton nafasi ya kuwaadhibu vilivyo. Mabao ya Brighton inayonolewa na Chris Hughton, yalifungwa na Glenn Murray, Shane Duffy na Pascal Gross huku la kufutia machozi la United likifungwa na Romelu Lukaku.
Wachambuzi wa soka wa England, Gary Neville na Graeme Souness wamerusha madongo kwa Bailly, ambaye pia alicheza hovyo na kusababisha penalti iliyozaa bao la tatu, wakisema kuwa alionekana kama mtu aliyekuwa kwenye mapumziko uwanjani.
Pia, waliponda kiwango kilichoonyeshwa na United kwenye mchezo huo, hasa safu ya ulinzi ambayo haikuwa mchezoni na kuruhusu mabao ya kizembe.