WANAPAGAWISHA: Kila wanachofanya mademu hutamani kukijua popote

ASIKWAMBIE mtu, wapo baadhi ya nyota wa kike nchini wanapagawisha mashabiki wa kiume kutokana na kujaliwa mvuto wa sura na maumbile yao matata. Mastaa

kama Wema Sepetu, Irene Uwoya, Jacquiline Wolper, Sanchi, Aunty Ezekiel, Shamsa Ford, Wellu Sengo, Shilole, Snura Mushi, Linah na hata Vanessa Mdee ni baadhi tu wadada wakali wanaowatoa udenda mashabiki wa kiume.

Kwenye maonyesho yao ama chochote wanachotupia kwenye mitandao au kazi wanazoshiriki zikitoka zinagombewa kwa sababu tu ya mvuto wao.

Lakini sasa kumbe hata mashabiki wa kike nao kuna watu wao wanaowazimia na kuwafuatilia kwa kila wanachokifanya iwe ndani ama nje ya sanaa wazifanyazo.

Mwanaspoti inakuleta wasanii watano wa kiume ambao wanawachizisha mashabiki wa kike kutokana na mvuto wao wa sura na muonekano wao, mbali na kazi zao zinazowapagaiwisha hata mashabiki wa kiume.

DIAMOND PLATNUMZ

Staa huyu anatajwa kama mmoja wa waimbaji wanaofuatiliwa kwa karibu na mashabiki wa kike kokote aliko. Kila analofanya Baba Tiffah, linafuatiliwa kwa karibu na mashabiki wa kike kutokana na mvuto mkubwa alionao kwao.

Ukiacha umbile lake lililojaa kimazoezi, umahiri wake wa kuimba nyimbo za mapenzi zinazogusa mitima ya mademu, lakini pia umatemate alionao Diamond na sarakasi zake ya kuwagonganisha wanawake kumemfanya awe na mvuto zaidi.

Katika kufuatilia akaunti za kurasa za mitandao ya kijamii, Diamond anafunika kwa kuwa na wafuasi wengi wa kike, wakati mwingine hata kununua ugomvi usiowahusu ilimradi kuonyesha namna gani wanavyomzimikia na kufuatilia Mond.

Diamond pia anapagawisha mashabiki kwa namna anavyojua kujiachia jukwaani akitumbuiza, huku akiwa ni kinara wa muziki wa kizazi kipya mwenye mafanikio makubwa ya kisanii nchini kwa sasa akitamba hadi anga za kimataifa.

ALI KIBA

Mpinzani mkubwa kwa Diamond ni Ali Kiba. Jamaa naye ni kati ya waimbaji wa kiume wanaozimikiwa na mashabiki wa kike, kiasi kuna wakati wanaamua kujibu mashambulizi kutoka kwa wapinzani wao ili mradi kumtetea Kiba.

Staa huo wa Mvumo wa Radi, ukiondoa mvuto wa sura yake na umbile lake la kimichezo, pia sauti yake imekuwa ikiwapagaiwisha mashabiki wengi wa kike na hasa apandapo jukwaani kutokana na gtabia yake ya kutawala jukwaa.

Kwa sasa Kiba ni mume wa mtu, lakini hiyo haiwafanyi mashabiki wa kike kuacha kumzimikia kwa sababu kazi yake ya sanaa inamweka karibu na watu hao ambao hata kwenye akaunti zake pia wanamfuata kwa wingi.

RAYVANNY

Nyota huyu anayetokea WCB ni kati ya wasanii wanaozimikiwa na mashabiki wa kike kwa muonekano wake wa sura na sauti tamu aliyojaliwa, sambamba na kufanya kazi nyingi na Diamond.

Hata wahenga walishasema ukikaa na muuza uturi naye nawe lazima unukie uturi, hivyo Rayvanny anazidi kung’ara kutokana na kufanya kazi na Mond na pia kipaji alichonacho mbali na muonekano wake.

HARMONIZE

Huyu naye anatokea WCB akipapatikiwa na mashabiki wa kike kutokana na sauti tamu aliyonayo, mbali na kuwa na mwili unaozimikiwa na mademu.

Nyimbo zake za mapenzi na anazoimba kwa kubembeleza zimemfanya Harmonize kukimbiza miongoni mwa wasanii walioibuka miaka ya karibuni katika muziki wa kizazi kipya.

JUX

Kuanzia umaridadi wake, sauti tamu na staili yake ya kuimba nyimbo za mahaba, zimemfanya Jux kuingia kwenye orodha hii ya wakali wanaozimikiwa na mademu.

Mwimbaji huyo ambaye ni mpenzi wa mkali mwingine wa muziki wa kizazi kipya nchini, Vanessa Mdee anatajwa kuwa na mvuto wa sura, mwili na sauti inayochizisha mashabiki wa kike sambamba na umahiri wake wa kucheza.

WENGINE

Ukiondoa wasanii hao , pia orodha haijawaacha nyuma, Gabo Zagamba anayetajwa kuzimikiwa kwa umahiri wake wa kuigiza na umbile alilonalo, kwani jamaa kakata hewa kiroho mbaya.

Rammy Galis, mkali wa filamu naye anatajwa kuwapagawisha mashabiki wa kike kwa mvuto wa sura na muonekano wake, mbali na uigizaji wake, kama ilivyo wa Ray Kigosi, Rich Mavoko, Ben Kinyaiya na mkongwe Dully Sykes a.k.a Mr Misifa.