SIMBA TAIFA KUBWA

MABINGWA wa soka nchini, Simba inajiandaa kuadhimisha siku malumu ya klabu hiyo maarufu kama Simba Day huku mashabiki wake wakiwa na shauku ya kuwaona nyota wao waliosajiliwa msimu huu.
Maadhimisho hayo yanayofanyika kila Agosti 8, ni maalumu kwa ajili ya utambulisho wa kikosi na jezi mpya za msimu kwa timu ya Simba, sambamba na kutoa tuzo kwa wadau wake.
Huu ni mwaka wa tisa tangu Simba Day ilipoanzishwa mwaka 2009 na uongozi wa enzi hizo chini ya Hassan Dalali 'Field Marshal' na Katibu Mkuu, Mwina Kaduguda 'Simba wa Yuda'.
Kina Dalali waliasisi siku hiyo ili kukutanisha wana Simba wote bila kujali ni nani ili kupanga mikakati ya maendeleo kwa timu yao kabla ya kugeuzwa mahususi kutambulisha kikosi na jezi za msimu mpya ikiambatana na mechi maaluma ya kirafiki.
Kwa wanaokumbuka ni mwaka mmoja tu wa 2014 tamasha hilo la Simba Day lilishindwa kufanyika Agosti 8 na kusogezwa mbele kwa siku moja, lakini miaka yote hufanyika Nane Nane.
Hata mwaka huu kama miaka mingine tamasha hilo litafanyika Agosti 8 likipambwa na burudani mbalimbali, sambamba na kutambulishwa kwa kikosi na jezi mpya za msimu wa 2018-2019.
Simba inalifanya tamasha hilo wiki moja tu kabla ya mchezo wao wa Ngao ya Hisani dhidi ya Mtibwa Sugar ili kuzindua msimu mpya wa Ligi Kuu Bara inayoingia mwaka wa 53.
Wanasimba wakijiandaa kufanya tamasha hilo linaloenda sawia na miaka 82 tangu klabu yao iasisiwe rasmi mnamo mwaka 1936 Mwanaspoti inakuletea baadhi ya rekodi za kusisimua za Simba zilizosababisha kupachikwa jina la TAIFA KUBWA.