Msuva kukiwasha kwa ES Setif

Muktasari:

Mechi hiyo inataraji kuwa na upinzani mkali kwa Difaa kutokana na wenyeji ES Setif kutaka ushindi huo ili kujiondoa mkiani mwa Kundi B wakiwa bila ya pointi.

Setif, Algeria. Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva kesho atakiongoza kikosi chake cha Difaa El Jadidi ugenini dhidi ES Setif kwenye Uwanja wa8 May 1945 jijini Setif.
Msuva watakuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha wanapata ushindi ili kujiweka vizuri katika kundi hili.
 Mechi hiyo inataraji kuwa na upinzani mkali kwa Difaa kutokana na wenyeji ES Setif kutaka ushindi huo ili kujiondoa mkiani mwa Kundi B wakiwa bila ya pointi.
Klabu hiyo ya Morocco, Difaa ilianza kwa kulazimisha sare 1-1 ugenini na MCA kabla ya kufungwa 2-0 nyumbani na Mazembe hivyo watalazimika kushinda mechi ya kesho ili kujiweka vizuri.
Difaa imeimarisha kikosi chake kwa kumsajili mshambuliaji Nigeria, Athony Okpotu ambaye anategemea kuanza katika mchezo huo.
Miamba hiyo ya Algeria ilianza kampeni yao msimu huu kwa kufungwa 4-1 ugenini na TP Mazembe, kabla ya kuchapwa 1-0 na ndugu zao MC Alger kabla ya mapumziko ya kupisha Kombe la Dunia 2018.
Mwamuzi wa Gambia, Bakary Gassama ndiye atakayechezesha mechi hiyo ya mjini Setif, wakati mchezo mwingine wa Kundi B utawashudia vinara  Mazembe wakiwavaa MCA jijini Lubumbashi.