Kiraka kuvaa buti za Kessy

Muktasari:

  • Kessy hajasaini mkataba mpya, pia hajajiunga na timu sawa na mkongwe Kelvin Yondani wanaoachwa kwenye msafara wa timu hiyo unaoenda Kenya kuifuata Gor Mahia kwa mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

BEKI wa Yanga, Hassan Ramadhan ‘Kessy’ inaelezwa bado amekaza akitaka Sh70 milioni ili asaini mkataba mpya, lakini mabosi wake wanapiga hesabu ndefu na sasa anaweza kupoteza nafasi kwani kuna kiraka mpya anataka kuletwa.

Kessy hajasaini mkataba mpya, pia hajajiunga na timu sawa na mkongwe Kelvin Yondani wanaoachwa kwenye msafara wa timu hiyo unaoenda Kenya kuifuata Gor Mahia kwa mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Hata hivyo tangu wiki iliyopita mabosi hao walishaanza maandalizi ya kumpoteza Kessy kwa kufanya mazungumzo na Boniface Maganga wa Mbao FC ili aweze kuitumikia timu hiyo.

Yanga imefungua mazungumzo na Mbao ya kumsajili beki huyo anayemudu kucheza nafasi nyingine mbele ili kuziba nafasi ya Kessy kama ataendelea kusumbua.

Akili ya mabosi wa Yanga baada ya kushauriana na makocha wao ni kutafuta beki mwingine atakayesaidiana na Juma Abdul ambaye bila hata kusaini mkataba mpya, ameshajiunga na timu.

Yanga hawakutaka kutafuta beki wa nguvu sana kufuatia msimu ujao kutoshiriki michuano ya kimataifa zaidi ya mechi za Ligi Kuu na Kombe la FA tu.

Mbali ya Abdul wengine ambao wameshajiunga na Yanga bila kusaini mikataba mipya ni kipa Beno Kakolanya na beki Andrew Vincent Dante ambao Mwanaspoti linafahamu wameshakubaliana kila kitu na uongozi wa klabu yao kuja kusaini mikataba mipya mara baada ya kurejea kutoka Kenya.

Msafara huo wa Kenya utahusisha makipa Youthe Rostand na Kakolanya, huku mabeki wakiwa ni Abdul, Mwinyi Haji, Gadiel Michael, Shaibu Abdallah ‘Ninja’, Dante, Said Makapu na Pato Ngonyani. Wengine ni Papy Kabamba Tshishimbi, Emmanuel Martin, Geofrey Mwashiuya, Amissi Tambwe, Juma Mahadhi, Pius Buswita, Said Mussa, Ibrahim Ajibu, Yohana Mkomola, huku Matteo Anthony akiwa hatihati kama rafael Daudi mwenye kadi mbili za njano, hivyo ataenda.

Ngassa, Makambo wakwama

Makosa ya kiutendaji ya Yanga yameiweka timu hiyo katika nafasi ngumu ya kuwakosa nyota wapya katika mechi mbili za makundi dhidi ya Gor Mahia kufuatia kuchelewa kutuma majina ya wachezaji watatu waliotakiwa kuongezwa.

Taarifa kutoka ndani ya Yanga zinasema benchi la ufundi lilipanga kuwaongeza viungo Deus Kaseke, Mrisho Ngassa na straika Heriter Makambo, ila viongozi walichelewa kuyatuma majina Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) linalotaka ili mchezaji acheze mchezo unaofuata jina lake linatakiwa liwasilishwe kwao siku 14 kabla ya tarehe ya mechi husika.

Kukosekana kwa nyota hao ni wazi kutaiumiza Yanga iliyomhitaji Makambo kuziba nafasi ya Obrey Chirwa aliyetimkia Misri.