Real macho yote kwa Neymar, Hazard

Muktasari:

Wakati uvumi ukizidi kukolea kuwa Real inawafukuzia mastaa wawili Neymar kutoka PSG na Eden Hazard wa Chelsea, Rais wa Klabu hiyo Florentino Perez, amekiri kuwa Neymar ni mchezaji wa kwanza wanayemuhitaji na wapo tayari kumsajili kwa gharama yoyote.

Madrid, Hispania. Klabu ya Real Madrid imeweka wazi kuwa ipo katika mkakati wa kumsajili mchezaji atakayechukua nafasi ya ‘Galacha’ wao Cristiano Ronaldo aliyeihama timu hiyo na kujiunga na Juventus ya Italia.

Wakati uvumi ukizidi kukolea kuwa Real inawafukuzia mastaa wawili Neymar kutoka PSG na Eden Hazard wa Chelsea, Rais wa Klabu hiyo Florentino Perez, amekiri kuwa Neymar ni mchezaji wa kwanza wanayemuhitaji na wapo tayari kumsajili kwa gharama yoyote.

Alisema bila kificho Neymar ndiye mchezaji bora atakayechukua nafasi inayoachwa wazi na mastaa waili walioitawala Dunia katika muongo mmoja uliopita Ronaldo na Lionel Messi.

“Tunadhani anastihili kwa sababu tumeona uongozi wake dimbani, licha ya umri wake mdogo lakini amefanya vizuri tangu ameteuliwa kuiongoza Brazil, tunaamini anaweza kuwa msaada mkubwa kwetu ndani ya uwanja,” alisema Perez.

Alisema wanajiandaa kuomba kukutana na viongozi wa Paris Saint-Germain ili waweze kuwashswishi wakubali kumuachia mchezaji huyo waliyemsajili mwaka jana kutoka Barcelona kwa Euro 222 milioni.

Alijitapa kwamba anaaimini mchezaji huyo anafurahia kuvaa jezi ya Real Madrid, lakini hawajui iwapo PSG itaendelea na msimamo wake wa kutotaka kumuuza kwa kiasi chochote cha fedha.

Kwa upande wa Hazard, alisema mchezaji huyo ambaye mkataba wake wa kuitumikia Chelsea utamalizika 2020 binafsi anataka kuihama timu yake na kuichezea Real Madrid hivyo anadhani kuna wepesi na jambo hilo litaanza kushughulikia baada ya kumalizika kwa fainali za Kombe la Dunia Jumapili hii.

Hazard ataiongoza Ubelgiji kucheza mechi ya kusaka mshindi wa tatau dhidi ya England baada na kufungwa 1-0 na Ufaransa katika nusu fainali.