#WC2018: Wamesababisha mshangao Russia

KABLA ya kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea kule Russia, kuna nchi zilipewa nafasi kubwa ya kutamba kutokana na vikosi vyao kuwa na mastaa wenye majina makubwa.

Nchi kama Brazil, Ujerumani, Ufaransa na nyingine kadhaa zilitajwa kwamba zitatamba. Kisa zina mastaa wenye majina makubwa.

Lakini, kuna nchi zilipewa nafasi ndogo ya kutamba licha ya kuwa na wachezaji mahiri kwenye vikosi vyao. Wachezaji waliopo kwenye vikosi hivyo mara zote hawapewi sifa wanazostahili na ndio maana hata nchi zao zilionekana kwamba zingefanya vibaya, lakini mambo yamekuwa tofauti baada ya kipute cha Russia kuanza rasmi. Wafuatao wamefanya makubwa hadi sasa kwenye fainali hizo.

5. Denis Cheryshev

na Russia

Wenyeji Russia walionekana chamtoto kutokana na historia yao. Ni kweli, Russia si mahiri kwenye soka la kimataifa, lakini kwenye fainali hizi Warusi wameonekana kuwa moto kweli kweli na kufunga mabao manane katika mechi mbili. Waliichapa Saudi Arabia 5-0 na kisha Misri 3-1.

Denis Cheryshev ndiye anayeshikilia makali ya kikosi hicho akiwa ameshafunga mara tatu na kuisaidia Russia kutinga hatua ya 16 Bora mapema tu baada ya mechi mbili.

4.Granit Xhaka na Uswisi

Baada ya kupangwa na Brazil kwenye kundi moja, ni wazi Uswisi walikuwa wakipewa nafasi ndogo licha ya kikosi chao kuwa na mastaa wengi makini akiwamo kiungo wa Arsenal, Granit Xhaka.

Kwa sababu walipangwa na Brazil, Uswisi walipewa nafasi finyu ya kufanya vizuri kwenye fainali hizo, lakini waliibana Brazil na kutoka nao sare na kisha wakaichapa Serbia kwenye mechi ya pili na hivyo kujiweka kwenye nafasi nzuri kabisa ya kutinga hatua inayofuata. Uswisi ya Xhaka sasa itacheza Costa Rica.

3.Luka Modric na Croatia

Baada ya kusikika tu kwamba Croatia wamepangwa kwenye kundi moja na Argentina, basi wengi walichokuwa wakiamini ni kwamba ingemaliza ya pili kwenye kundi hilo. Hawakuwa wakijali kwamba kikosi hicho kina mastaa kibao wa maana akiwamo Luka Modric.

Mambo yamebadilika na Croatia ndiyo timu iliyofuzu kwenye kundi hilo hadi sasa, tena wakiichapa Argentina 3-0. Modric ni staa mkubwa kwenye soka la dunia na hilo limeifanya Croatia kutamba kwenye fainali hizo kutokana na huduma yake maridadi akihusika pia kwenye mabao.

2.Cristiano Ronaldo

na Ureno

Ureno siku zote imekuwa ikipewa nafasi ndogo kwenye michuano mikubwa kwa sababu ya wachezaji wake. Lakini, kwa kuwa ina Cristiano Ronaldo, siku zote inakuwa haitabiriki.

Ronaldo ni kama mvinyo, kwamba unakuwa mtamu zaidi kwa kadiri unavyozidi kuwa na umri mkubwa. Si tu alifunga mabao matatu katika mechi moja, lakini Ronaldo amefunga mara nne na kuwa mmoja wa wanaoongoza kwa mabao kwenye fainali hizo na sasa Ureno imeanza kuwa timu tishio.

1.Sadio Mane na Senegal

Timu nyingi za Afrika zilipewa nafasi finyu ya kutamba kwenye fainali za Kombe la Dunia huko Russia. Kwa mwaka huu, Misri ndio waliokuwa wakipewa nafasi kubwa kwa upande wa timu za Afrika, lakini wenyewe baada ya mechi mbili tu, wameshaaga michuano.

Senegal hawakuwa wakipewa nafasi licha ya kuwa na staa wa kiwango cha juu kama Sadio Mane. Simba wa Teranga hao wamefanya maajabu yao baada ya kushinda mechi yao ya kwanza dhidi ya Poland ya Robert Lewandowski.