Mara paap! Singida yarudi sokoni kusaka straika

KOCHA Mkuu wa Singida United, Hemed Morocco ameweka wazi michuano ya SportPesa Super Cup imemwonyesha anahitaji kurejea tena sokoni kusaka straika.

Singida United imecheza mechi mbili za michuano hiyo dhidi ya AFC Leopards na Gor Mahia bila kufunga bao lolote, jambo ambalo limemgusa Morocco na kusema sasa wanahitaji straika wa maana.

Morocco alisema Singida imekuwa na tatizo la straika hata kabla hajajiunga na timu hiyo hivyo hawezi kurekebisha kwa siku mbili, lakini ni wazi kuwa wanahitaji mfungaji wa maana.

“Siyo jambo zuri hata kidogo kucheza dakika 180 bila kufunga bao. Tunahitaji mastraika wengine ambao watakuwa na uwezo mkubwa zaidi, nitarejea sokoni kutazama nani anaweza kutusaidia,” alisema Morocco.

Akizungumzia kuondoshwa kwenye nusu fainali ya michuano hiyo ya SportPesa, alisema ni changamoto za kiufundi lakini walizidiwa pia utimamu wa mwili na Gor Mahia walioshinda 2-0.

“Mvua ilipoteza msisimko wa mchezo, tulijaribu kupambana lakini wenzetu walikuwa fiti zaidi, walituzidi kwa kiasi fulani,” alisema.