Singida yazuia usajili wa Kagere Yanga

Sunday June 10 2018

 

By GIFT MACHA

MABAO mawili aliyofunga straika wa Gor Mahia, Meddie Kagere dhidi ya Singida United katika michuano ya SportPesa Super Cup huenda yakatibua mipango yake yote ya kujiunga na Yanga.

Kagere anaelekea ukingoni mwa mkataba wake na Gor Mahia na Yanga na Azam zimehusishwa na nia ya kutaka kumchomoa kwenye kikosi hicho cha mabingwa wa Ligi Kuu Kenya.

Straika huyo aliyezaliwa Uganda lakini anaitumikia timu ya taifa ya Rwanda, ndiye anaongoza kwa mabao kwenye michuano ya SportPesa Super Cup akiwa amefunga mara tatu mpaka sasa na kufuatiwa na Allan Wanga wa Kakamega Homeboys mwenye mabao mawili.

Kocha Mkuu wa Gor Mahia, Dylan Kerr alisema ni kweli wanakabiliwa na wakati mgumu wa kumbakisha straika huyo, lakini hawawezi kumruhusu aondoke kwa sasa mpaka mkataba wake utakapomalizika mwishoni mwa mwaka huu.

Kerr alisema Kagere yuko kwenye mipango yake ya sasa na ya baadaye, ila hatakuwa na uwezo wa kumzuia mkataba wake utakapomalizika, lakini kwa sasa timu inayomtaka iandae fungu kubwa la fedha.

Alisema ili kumwachia straika huyo, ni lazima wapate fedha ambazo zinaweza kuwasaidia kununua straika mwingine wa maana.

“Amecheza vizuri dhidi ya Singida United. Amefanya kile ambacho straika anapaswa kufanya, ni habari nzuri kwetu,” alisema Kerr.

“Baada ya kiwango chake hiki siwezi kumruhusu aondoke, yuko kwenye fomu. Bado yuko kwenye mipango yangu hapa, tunatazama namna ya kumpatia mkataba mpya,” alisema Kerr.

“Ila mkataba wake unamalizika mwishoni mwa mwaka, anaweza kuondoka baada ya hapo kama ataamua kufanya hivyo. Kwa sasa siwezi kumruhusu, labda kama timu itakayokuja ina ofa nzuri,” alisema kocha huyo wa zamani wa Simba.

CAF YAMKWAMISHA MAVUGO

Katika hatua nyingine, kitendo cha straika wa Simba, Laudit Mavugo kuitumikia timu hiyo kwenye mechi za Kombe Shirikisho Afrika kimekwamisha usajili wake ndani ya Gor Mahia.

Kerr alifichua Mavugo ni miongoni mwa mastraika ambao walikuwa kwenye mipango yake kwa sasa, lakini hawezi kumsajili tena kwani hawezi kucheza kwenye mechi za kimataifa.

“Nilikuwa natamani aje hapa, ni straika mzuri lakini hatuwezi kumwongeza kwenye mechi za kimataifa, ameichezea Simba tayari,” alisema Kerr.