Huku kuna Okwi, kule Salamba mtakoma tu

KAIMU kocha mkuu wa Simba, Masoud Djuma amewatazama mastraika wapya wa timu hiyo, Adam Salamba na Mohammed Rashid kisha akasema jambo.

Djuma amesema nyota hao wameonyesha uwezo mzuri mpaka sasa, lakini wanakabiliwa na changamoto za hapa na pale hasa kuzoea mazingira ya timu mpya.

Salamba amejiunga na Simba akitokea Lipuli ya Iringa na juzi Alhamisi alicheza kwa dakika 35 wakati Simba ikiiondosha Kakamega Homeboys kwenye nusu fainali ya SportPesa Super Cup.

Rashid ametua Simba akitokea Prisons ya Mbeya aliyoifungia mabao 10 msimu uliopita, na ameanza kwenye mechi mbili za michuano hiyo dhidi ya Kariobangi Sharks na Kakamega Homeboys.

Djuma ambaye anakaimu nafasi ya kocha mkuu baada ya Mfaransa, Pierre Lechantre kuondoka, amesema inawezekana mastraika hao wangeaza kucheza sambamba na John Bocco ama Emmanuel Okwi wangefanya vizuri zaidi.

“Ni kweli, kuna wakati unaona kabisa ni ugumu tu wa kuzoea timu. Pengine wangekuwa wanacheza na Okwi na Bocco wangefanya vizuri zaidi.

“Ila hili ni soka, lolote linaweza kutokea, wanaweza kucheza sambamba nao bado isiwe hivyo. Muhimu ni kwamba ni wachezaji wazuri, nimewaona kabla hawajaja hapa Simba na baada ya kuja, wataisaidia timu,” alisema Djuma.