Kaheza ajipanga Simba

Muktasari:

Kaheza ambaye anapenda kuvaa jezi namba 10 uwanjani kwa sababu ya mapenzi yake kwa Rivaldo, amesaini mkataba wa miaka miwili baada ya mfanyabiashara na mwanachama wa Simba, Mohammed Dewji 'Mo' kumtumia tiketi ya ndege kutoka Songea awahi haraka Dar es Salaam kwa ajili ya kukamilisha zoezi hilo

Dar es Salaam: Yule straika wa Majimaji FC aliyesumbua sana kwenye msimu wa Ligi Kuu Bara unaomalizika kesho Jumatatu, Marcel Kaheza 'Rivaldo' amesaini mkataba wa awali na Simba kwa ajili ya msimu ujao ambapo sasa ameshaanza mikakati mizito ya namna atakavyoishi kikosini hapo.

Kaheza ambaye anapenda kuvaa jezi namba 10 uwanjani kwa sababu ya mapenzi yake kwa Rivaldo, amesaini mkataba wa miaka miwili baada ya mfanyabiashara na mwanachama wa Simba, Mohammed Dewji 'Mo' kumtumia tiketi ya ndege kutoka Songea awahi haraka Dar es Salaam kwa ajili ya kukamilisha zoezi hilo.

Inadaiwa 'Mo' amefanya zoezi hilo kwenda haraka kutokana na baadhi ya timu kama Azam FC ambayo itakuwa chini ya Kocha Mkuu Mholanzi Hans Pluijm pamoja na Singida United kumwania.    

Mtu wa karibu wa Kaheza amesema, jamaa sasa anajipanga na hataki kurudia makosa yale aliyoyafanya miaka ya nyuma hadi akatolewa kwa mkopo: "Unajua baada ya kufanikisha zoezi hilo, Kaheza akili yake yote ni namna atakavyopambana apate namba ya kudumu kikosini hapo."

Kabla ya kujiunga na Majimaji, Kaheza aliichezea timu hiyo ya Simba ya vijana chini ya miaka 20 na baadaye alipandishwa ya wakubwa, kutokana na ushindani wa namba uliopo hapo, wakaamua kumpeleka kwa mkopo katika timu hiyo.

Kaheza amefanikiwa kufunga mabao 13 katika kipindi cha ligi kuu msimu huu na ni miongoni mwa wachezaji waliofanikiwa kutwaa Tuzo za kila mwezi zinazotolewa na wadhamini Vodacom, akichukua mwezi Aprili.