Gabo: Urasimu kikwazo kwa filamu nchini

Muktasari:

  • Akizungumza na MCL Digital, Gabo alisema taratibu za hapa nchini katika kutumia sare za jeshi hilo ni ngumu jambo lililomfanya kwenda kufanyia kazi yake iliyohitaji watu waliovaa kipolisi nchi jirani kutokana na wao kuchukulia kawaida jambo hilo kwa wasanii wao wanapozihitaji.

Dar es Salaam. Mwigizaji bora wa kiume wa Tuzo za ‘Sinema Zetu International Film Festival Award (SZIFF)’2018, Ahmed Salim ‘Gabo Zigamba’, amesema amelazimika kwenda kupiga picha nchi za nje kwa ajili ya kukosa sare za Jeshi la Polisi hapa nchini.
Akizungumza na MCL Digital, Gabo alisema taratibu za hapa nchini katika kutumia sare za jeshi hilo ni ngumu jambo lililomfanya kwenda kufanyia kazi yake iliyohitaji watu waliovaa kipolisi nchi jirani kutokana na wao kuchukulia kawaida jambo hilo kwa wasanii wao wanapozihitaji.
“Kikweli nchi yetu kuna mambo inayafanya kuwa magumu kwa wasanii bila sababu katika kuzifanya kazi zao ziwe halisi, mfano ishu ya kupata sare za Jeshi la Polisi hapa nchini imekuwa ngumu na hata ukitaka kushona zifanane na wao, utapewa masharti kibao, hivyo nimeamua kwenda kupigia vipande vya picha vinavyohitaji watu waliovaa sare zao nchi nyingine.
“Japokuwa haileti picha nzuri kwa kuwa ukweli ni kwamba sisi tuna sare zetu, lakini huko utaona watu wamevaa hadi sare za Polisi za Jeshi la nchini Afrika Kusini na hivyo tunajikuta tunawatangaza wenzetu katika suala zima walivyojizatiti kiulinzi,” alisema Gabo.
Hali hiyo a;osema haipo tu kwa polisi bali hata kwa upande wa kutumia hifadhi za Taifa zikiwemo mbuga za wanyama na makumbusho mbalimbali ambapo hutakiwa kulipia hela nyingi wakati uwezo wao ni mdogo.
Kwa hili Gabo alisema serikali inatakiwa iwatumie wasanii katika kutangaza utalii ambao wana nafasi kubwa ya kufikisha ujumbe kwa  watu wengi kwa wakati mmoja na pia ingepunguza gharama ambazo Wizara ya maliasili imekuwa ikitumia ikiwemo kusafirisha watu nje ya nchi, kuandaa vipeperushi na mambo mengine.
MCL Digital, ilimtafuta Msemaji wa Jeshi la Polisi, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP), Barnabas Mwakalukwa,  kuweza kulisemea hilo, ambapo alidai kwamba wanasanii hao ili waweze kuruhusiwa kupata sare hizo au kuzishona ni lazoma waandike barua kwa Mkuu wa Jeshi hilo(IGP) au Mkuu wa Nchi ambaye ndiye Amiri Jeshi Mkuu.
“Jamani kila kitu kina utaratibu wake, hata ofisini kwako siwezi kuja tu na kuingia kwa kuwa mimi tu ni Polisi, ni lazima utataka kitambulisho na mambo mengine kujidhihirisha kama ni Polisi, vivyo hivyo wasanii wanapaswa kufuata sheria na kanununi zilizowekwa katika kutumia sare zetu,”alifafanua Kamishna Mwakalukwa.
Alieleza kuwa kwa mujibu wa sheria ni makosa kukutaa na sare za mtumishi wa umma, hivyo wasanii wajue kama watafanya hivyo bila kibali sheria itachukua mkondo wake na kuwataka kuacha kulalamika bali wafuate sheria.
“Ieleweke kwamba endapo Jeshi litaruhusu kila mtu kuvaa sare zake vile wanavyotaka kuna hatari ya baadhi ya watu kutumia mwanya huo kuzitumia vibaya katika kutenda uhalifu na pia ni vema wasanii wakaomba kupata mafunzo ya namna ya kuigiza nafasi za upolisi ili kuweza kuleta uhalisia,” alisema Kamishna Mwakalukwa.