Tusiwakatishe tamaa, lakini pia tusiwalaumu watakapofanya vibaya

TIMU ya taifa ya Tanzania kwa ajili ya Michezo ya Madola ipo kambini kwa sasa ikijiandaa na safari ya kwenda katika Michezo ya Madola itakayoanza Aprili 5-14 nchini Australia.

Tanzania inatarajia kuwakilishwa na timu itakayohusisha wachezaji wa timu ya riadha, ngumi, kuogelea na mpira wa meza katika mashindano hayo.

Hata hivyo, ni ukweli usiopingika kuwa, jicho la Watanzania wengi lilikuwa zaidi kwenye timu ya riadha na ngumi kutokana na ukweli michuano hiyo ndiyo yenye rekodi ya kubeba medali. Sio kwamba kuogelea ama mpira wa meza ni wabaya, lakini katika ushiriki wao kwenye michuano hiyo haujawahi kuwa na mafanikio

makubwa kwani mara nyingine timu hizo zimekuwa zikitolewa mapema.

Rekodi zimekuwa zikiwabeba timu za ngumi na riadha katika michezo hiyo kwani ndizo angalau zimekuwa zikiitoa kimasomaso Tanzania katika michuano ya kimataifa kama hiyo ya Madola, Olimpiki na hata Michezo ya Afrika.

Ukiangalia rekodi ya ngumi kwa miaka ya karibuni ya ushiriki wa michuano ya kimataifa, inakatisha tamaa na tumaini pekee la Australia kubaki mikononi mwa Riadha bila kutaka kuficha ukweli.

Hata hivyo, kuna kitu kimetokea kwenye timu hizo kabla hata hawajaanza kusafiri kwenda Australia, ngumi imeteua mabondia wanne bila hata mabondia wake kushiriki mashindano ya kimataifa ili kupima viwango vyao. Hilo hatutapenda kuliongelea sana, lakini nako kwenye riadha mchezo tegemeo la Tanzania katika Madola kumeingia mdudu.

Wanariadha karibu 10 tegemeo katika michezo hiyo ya Madola wameondolewa kwa maelezo ya kwenda kupata mafunzo maalumu ya kijeshi.

Uamuzi huo wa kuwaengua wachezaji hao sio tu umewavuruga wachezaji wengine wa timu hiyo, lakini hata wadau wa riadha wameshindwa kuelewa kuna kitu gani nyuma ya uamuzi huo. Wachezaji walioenguliwa ni tegemeo kwa taifa na hata wadau wanaamini wangeweza kurejea na medali kwa sababu ya uwezo wao.

Hata hivyo, msimamo wa waajiri wao, umekwamisha wachezaji hao kurejea kikosi cha taifa kwa sababu muda wa usajili umepita, lakini hili ni pigo kubwa kwa timu yetu na haitashangaa kuona Tanzania ikirejea mikono mitupu kutoka Australia.

Tunafahamu kuwa, wanariadha wengine wa timu hiyo watalibeba jukumu la taifa,lakini hata wao wataenda Australia wakikosa kujiamini kwa kutambua kuwa nyota walioondolewa wakiwa kama kichocheo chao cha kufanya vizuri zaidi.

Wakati msafara wa timu hiyo ya Tanzania ukitarajiwa kuondoka Machi 27, lakini ukweli Watanzania wameanza kuikatia tamaa mapema baada ya kutambua kuwa, haitakuwa na mtu kama Emmanuel Giniki, Alphonce Simbu, Magdalena Shauri, Fabiano Joseph, Angelina Tserre na wenzao.

Papo hapo, ikumbukwe kuwa, juzi tu, mwanariadha mwingine muhimu, Augustino Sulle alitimuliwa kwa sababu ya utovu wa nidhamu, kitu kinachozidi kuipa wakati mgumu timu ya Tanzania katika michezo hiyo ya Australia.

Inawezekana hisia za wadau ni sahihi, kutokana na ukweli kuondolewa kwa nyota 10 wa mchezo huo katika timu ya taifa ni kuidhoifisha timu, lakini pia tusiwakatishe tamaa wanamichezo wengine watakaokuwa kwenye msafara huo.

Tunaamini hii itakuwa nafasi nzuri kwao kuthibitisha kuwa wanaweza na kuibeba Tanzania, lakini ikitokea wakachemsha wasilaumiwe, kwa sababu ni kama tumejitengenezea mazingira ya kujinyima medali wenyewe tangu mapema.

Tangu mzozo wa Simbu awe Madola ama aende London Marathoni, ilitosha kuthibitisha tulikuwa tunajitengenezea bomu la aina gani, hivyo kila mshiriki wa jambo la sasa lazima abebe lawama upande wake. Asitafutwe mchawi baadaye.

Lakini tunawakumbusha tu wachezaji waliosalia katika kikosi cha riadha wasaidiwe kuandaliwa kiasaikolojia ili kwenda kupambana, lakini ieleweke wazi kama timu haitarudi na medali kusiwe na wa kumlaumu kwa sababu Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) limejitahidi kadri inavyoweza kurejesha heshima ya mchezo huo. Mwanaspoti haitaki kumnyooshea mtu kidole kilichotokea, lakini imesikitishwa na kilichofanyika kwa kuzingatia kuwa ilifahamika mapema kwamba Tanzania itashiriki michuano hiyo na timu iliyotegemewa iliundwa na wanariadha hao, lakini kwa vile mwajiri ana mamlaka, hatuna namna zaidi ya kuwaachia wahusika wenyewe, huku tukiwatia moyo waliosalia.