Mkwara wa MO waipoteza Yanga

Monday December 11 2017

 

By MASOUD MASASI

HAPA Mwanza kuna kijiwe kimoja cha mashabiki wa kulialia wa Simba na Yanga kinaitwa bendera tatu, sasa bwana baada ya Bilionea Mohamed Dewji ‘MO’ kupewa Simba yake mashabiki wa Yanga wametoweka kijiweni hapo na kutokomea kusikojulikana.

Kijiwe hicho maarufu kipo katika Mtaa wa Rufiji katikati ya Jiji la Mwanza ambapo sasa mashabiki na wanachama wa Simba kila kukicha ni stori za MO tu ambazo zimewafanya Yanga kukosa cha kuzungumza.

MO Dewji alitangazwa mshindi wa zabuni ya uwekezaji klabuni hapo ambapo aliweka kiasi cha Sh20 bilioni kupata asilimia 50 ya hisa licha ya kwamba serikali imesisitiza kuwa atapewa 49 tu.

Kiongozi wa kijiwe hicho, Hassani Kaheshi alisema baada ya MO kupewa timu mambo yamekuwa magumu kwa wenzao wa Yanga kijiweni hapo kwani wanajua TP Mazembe mpya inakuja hapa Bongo.

“Sisi kama wanachama na mashabiki wa Simba Mwanza tumepata jeuri, wenzetu wa Yanga wamekosa cha kuzungumza kwani wanajua mziki unaokuja na sasa wanafika kwa machale kijiweni hapa,” alisema Kaheshi.

Hata hivyo, kiongozi huyo alisema wao kama mashabiki wa Simba Mwanza wanataka bilionea huyo aanze na kuboresha benchi la ufundi kwenye timu yao.

Pia, alisema Simba haina uwanja wa mazoezi, hivyo anatakiwa kuanza nao huku  pia akisajili wachezaji wenye kiwango kikubwa kutoka nje ya nchi.