Waafrika hawa wanakunja noti nyingi kinoma

Thursday October 12 2017

 

By FADHILI ATHUMANI

KATIKA hili hakuna ubishi, hata kama hautakubali. Bara la Afrika limebarikiwa, kuanzia kwenye mavazi, tamaduni, utajiri wa rasilimali, upendo, heshima, vipaji vya michezo hadi wanawake wazuri wenye miili ya kibantu. Tumebarikiwa kinoma.

Sifa za bara hili lililotoa watu waliotukuka kwa uadilifu wa kimataifa kama Simba wa Afrika, Hayati Nelson Mandela na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (Mungu azilaze roho zao mahali pema peponi), zimeenda pia katika soka, mchezo namba moja kwa kupendwa duniani.

Ijapokuwa Afrika haina rekodi za kutambia katika kutwaa Kombe la Dunia, lakini sifa na uwezo wa uzao wa Afrika umetamalaki kwenye ulimwengu wa soka, ndio maana kuna watu kama George Weah, Roger Milla, Jay Jay Okocha, Didier Drogba, Samwel Eto’o Fils, utakapoyataja majina yao ukiwa kona yoyote duniani, utakuwa umeitangaza Afrika.

Kwa vipaji vyao vikubwa vya soka, mastaa kadhaa kutoka Afrika wamejikuta wakiwa wachezaji muhimu kwenye klabu zao huku Ulaya na kwingineko, kiasi cha kulipwa fedha ndefu. Kuna wanaolipwa mshahara wa mwaka unaozidi bajeti ya wizara moja katika nchi yake ya Afrika.

Kukiwa na wimbi la mastaa kadhaa kuhamia China kunakoaminika kuwa kuna neema ya fedha, swali linaloumiza vichwa hivi sasa ni nani kati ya Waafrika wanaocheza ligi mbalimbali kote duniani anaoongoza kwa kulipwa fedha nyingi? Hapa Mwanaspoti linakupatia ‘Top Ten’ yao kwa jinsi wanavyolipwa fedha nyingi. Viwango hivi ni kwa wiki tu.

10. Victor Moses -

Chelsea (Pauni 50,000)

Mnigeria huyu anayekipiga pale Stamford Bridge, analipwa mshahara wa Pauni 50,000 kwa wiki. Winga huyu ni mtu muhimu katika kikosi cha mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu England ambapo kocha, Antonio Conte, anamtumia katika mfumo wake wa 4-3-2-1.

9. Emmanuel Adebayor - Istanbul Basaksehir (Pauni 58,000)

Mshambuliaji huyu wa zamani wa Arsenal, Manchester City, Tottenham na Crystal Palace ambaye ni raia wa Togo, kwa sasa anakipiga Istanbul Basaksehir ya Uturuki aliyojiunga nayo mwezi Januari. Emmanuel Adebayor, analipwa mshahara wa Pauni 58,000 kwa wiki.

8. Ahmed Musa - Leicester City (Pauni 60,000)

Mnigeria mwingine katika orodha hii ni Ahmed Musa. Musa anakipiga klabuni Leicester City anakolipwa kiasi cha Pauni 60,000 kwa wiki.

7. Kelechi Iheanacho – Leicester City

(Pauni 100,000)

Kuwasili kwa Gabriel Jesus kikosini Manchester City kulimaanisha jambo moja, kwamba nafasi ya Mnigeria Kelechi Iheanacho katika kikosi cha kocha, Pep Guardiola, ilikuwa finyu. Ikabidi aondoke Etihad.

Kwenye dirisha la usajili lililofungwa, Man City, ikaamua kumpiga bei straika huyo. Kwa sasa anakipiga Leicester City anakolipwa mshahara wa Pauni 100,000 kwa wiki.

6. Obafemi Martins - Shanghai Shenhua (Pauni 100,000)

Mmoja kati ya wachezaji wanaovuna pesa nyingi katika Ligi Kuu China ni Mnigeria, Obafemi Martins.

Martins anaingia katika nafasi ya sita kwenye orodha hii akiwa anaingiza mshahara wa Pauni 100,000 kwa wiki. Kwa sasa anaichezea Shangai Shenhua.

5. John Mikel Obi - Tianjin TEDA (Pauni 140, 000)

Baada ya kuitumikia Chelsea kwa zaidi ya miaka 11 ya mafanikio, hatimaye mapema mwaka huu klabu hiyo iliachana naye. Mnigeria huyu anayecheza nafasi ya kiungo, kwa sasa anakipiga klabuni Tianjin TEDA inayoshiriki Ligi Kuu China anakolipwa mshahara wa Pauni 140, 000 kwa wiki.

4. Samuel Eto’o

Fils- Antalyaspor

(Pauni 170,000)

Maisha yanaenda kasi sana aisee. Ni ngumu kuamini kuwa Mcameroon huyo ambaye ni staa wa zamani wa Barcelona, Inter Milan na Chelsea, kwa sasa anashika nafasi ya nne katika orodha ya mastaa wa Kiafrika wanaolipwa fedha nyingi.

Itakumbukwa kuwa mwaka 2013 baada ya kujiunga na Anzhi Makhachkala ya Urusi, Eto’o alikuwa ndiye mchezaji ghali zaidi Mwafrika ambapo alikuwa akitia kibindoni mshahara wa Euro 8 milioni kwa mwaka.

Kwa sasa straika huyu anamalizia soka lake Uturuki katika klabu ya Antalyaspor, anakolipwa mshahara wa Pauni 170,000 kwa wiki.

3. Odion Ighalo -

Changchun Yatai

(Pauni 190,000)

Katika nafasi ya tatu anasimama Mnigeria mwingine, Odion Ighalo. Mshambualiaji

huyu wa zamani wa Watford, kwa sasa yupo China anakoendelea kuvuna hela kwenye klabu ya Changhun Yatai inayomlipa mshahara wa Pauni 190,000 kwa wiki.

2. Yaya Toure -

Manchester City

(Pauni 220,000)

Mchezaji Bora wa Afrika wa mara nne, Muivory Coast Yaya Toure, yupo katika nafasi ya pili. Kiungo huyu wa Man City ambaye kwa sasa anasota kwenye benchi pale Etihad, analipwa mshahara wa Pauni 220,000 kwa wiki.

1. Asamoah Gyan -

Shanghai SIPG

(Pauni 227,000)

Maisha ni karata. Baada ya mambo kutomwendea vyema England, Asamoah

Gyan wala hakutaka kutumia nguvu nyingi, aliamua kusaka fedha. Kituo chake cha kwanza kikawa kule Falme za Kiarabu kabla ya kuhamia kwa Wachina mwaka 2015.