Simba yaizidi Zamalek, Enyimba

SIMBA imerudi anga za kimataifa na mwakani huenda ikaangukia mikononi mwa Zamalek ya Misri, Enyimba ya Nigeria ama Raja Casablaca ya Morocco katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Timu hizo na vigogo vingine vya soka barani Afrika zitashiriki michuano hiyo itakayoanza mapema mwakani, na Wekundu hao wanarudi anga hizo tangu mwaka 2013 waliposhiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na kisha kupotezwa jumla.

Katika kutambua kibarua kilichopo mbele yake na hasa kazi ya kuwapa raha mashabiki wa Simba, Kocha, Joseph Omog ameanza kusuka mipango kabambe ya ushiriki wa michuano hiyo na kama utatiki basi usiombe ukutane na Simba.

Simba itaanza kibarua chake mapema Februari na Omog alisema anatambua ana michuano hiyo ni migumu ikijumuisha timu zenye nyota wa kimataifa.

Hivyo katika kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa, ndio maana ameanza kujipanga mapema ili kuwaandaa vijana wake kuweza kukabiliana na changamoto iliyopo mbele yake. Akiamini itamsaidia kuwazidi ujanja wapinzani atakapopangwa nao kuusaka ubingwa wa michuano hiyo ya pili kwa ukubwa Afrika kwa ngazi ya klabu.

“Wachezaji nilionao wote ninaamini wanakidhi mahitaji ya mashindano hayo, ndio maana tumesajili wachezaji wengi wenye vipaji na wenye uzoefu wa michuano ya kimataifa.”

“Maandalizi makubwa ya kuelekea michuano hiyo nitaangalia tumepangwa na nani, lakini ukweli tunaanza mapema ili kuona hatukwami hatua za awali.

“Tukishajua tumepangwa na timu gani, nitajua tuweke kambi hapa nchini au nje kama tulivyofanya mwanzo wa maandalizi ya ligi,” alisema Omog.

“Kwa hiyo ratiba kamili ya michuano hii ya kimataifa ambayo tutakuwepo mwakani, nitaanza maandalizi yake mapema tena yatakuwa Desemba,” aliongeza.

KAMILI GADO

Omog alisema katika kikosi alichonacho msimu huu, haitaji kufanya usajili mkubwa kwenye dirisha dogo litakalofunguliwa rasmi Novemba 15.

“Mpaka hapa tulipofikia kikosi changu kipo vizuri na vijana nilionao wamefanya kazi nzuri na nitakuwa nao hadi mwisho wa msimu.

“Kama itatokea kufanya usajili sidhani kama utakuwa mkubwa kama nilioufanya mwanzo wa msimu huu, ila nitasajili wachezaji watatu au wawili si zaidi ya hapo,” alisema Omog na kuongeza: “Kuhusu kuwaacha baadhi ya wachezaji sidhani kama litatokea jambo hilo kwa sasa katika kikosi changu, kwani wachezaji wote nawahitaji na wapo katika mipango yangu.

“Kama kutakuwa na mchezaji, ambaye atakuwa na shida yake binafsi ambayo itayofanya ashindwe kubaki klabuni basi huyo nitampa baraka zote huko aendapo.”

VIGOGO

Katika michuano hiyo ya kimataifa, Simba ipo katika nafasi ya kukumbana na vigogo toka Afrika Kaskazini, Magharibi na hata Kusini.

Baadhi ya timu vigogo zilizoungana na Simba katika michuano hiyo ni Zamalek na Al Masry za Misri, Club Africain na US Ben Guerdane za Tunisia, Raja Casablanca ya Morocco, DC Motema Pembe ya DR Congo, Africa Sports ya Ivory Coast, Supersport na Cape Town City za Afrika Kusini, Enyimba ya Nigeria na Costa do Sol ya Msumbiji ambazo historia yake kwenye michuano ya kimataifa sio ya kitoto kabisa.