HISIA ZANGU: Ninawaza...sijui kama Msuva, Kichuya watajivua gamba kama Ronaldo

Muktasari:

Bahati nzuri kwa Ronaldo amezungukwa na wataalamu wanaoifahamu sayansi ya mpira wa miguu. Ilitazamiwa kwamba Ronaldo wa leo wa miaka 32 asingekuwa na kasi kama Ronaldo wa miaka 24.

WAKATI Chama cha Mapinduzi, CCM kitakapotimiza miaka 41 itakapofika Februari 5 mwakani, siku hiyo hiyo Cristiano Ronaldo atakuwa anatimiza miaka 33. Usimwone anafunga, umri umemtupa. Bahati nzuri hakudanganya miaka yake.

Bahati nzuri kwa Ronaldo amezungukwa na wataalamu wanaoifahamu sayansi ya mpira wa miguu. Ilitazamiwa kwamba Ronaldo wa leo wa miaka 32 asingekuwa na kasi kama Ronaldo wa miaka 24.

Wataalamu wa soka ndani ya Real Madrid sasa wameubadili mpira wake kabisa.

Katika mechi ya Jumamosi iliyopita dhidi ya Juventus pale Cardiff, Ronaldo alitupia mabao mawili yote akiwa ndani ya boksi.

Katika mabao 12 aliyofunga msimu huu wa Ligi ya mabingwa wa Ulaya, yote amefungia ndani ya boksi. Ronaldo ameambiwa asikimbie sana. Ni kweli.

Hata akiamua kukimbia sana na kupiga zile chenga za ‘baiskeli’ umri hauwezi kumruhusu. Ndio maana sasa hivi amerudi kucheza katikati na kuvizia kwa ustadi.

Staili yake ya ufungaji ya siku hizi ni ya uviziaji zaidi (goal poacher).

Zamani Ronaldo alikuwa akifunga zaidi kutokana na kasi yake kule kushoto, kisha anakatiza katikati ya uwanja, halafu anapiga mashuti makali. Ronaldo huyu kwa sasa ameondoka, amebakia Ronaldo mviziaji ambaye anafanya kazi yake kwa ukamilifu. Ni kama nyoka aliyejivua gamba aendelee kubaki kijana.

Ronaldo wa sasa anajua asimame wapi. Basi. Tengeneza taswira kichwani halafu fikiria mabao yote mawili aliyofunga dhidi ya Juventus. Amesimama katika nafasi akisubiri krosi za akina Luka Modric. Hakusumbuka sana, lakini kaibeba timu.

Hawa ndio wazungu wanaojua kukikamua kipaji mpaka dakika ya mwisho. Niliwahi kuandika ukurasa huu jinsi ambavyo wenzetu wanavyoweza kubadili mchezo wa wachezaji kulingana na umri.

Na ndio maana bado nashangaa ilikuwaje Shadrack Nsajigwa akastaafu akiwa beki wa kulia.

Aliondoka na nguvu zake. Hata kama hazikuwa nguvu za kufukuzana na mawinga, lakini alibakiwa na nguvu ambazo zingeweza kumwezesha kucheza katika eneo dogo kama ambalo Ronaldo anacheza leo.

Kwa mfano, nilimfahamu Nsajigwa akiwa kiungo mkabaji nikiwa shule.

Hii ni nafasi ambayo angeweza kumalizia nguvu zake na angeweza kucheza kwa miaka mitatu zaidi kwa sababu ukicheza kiungo wa eneo lake, haukimbii zaidi kuliko kucheza beki wa kulia.

Si katika kiungo tu. Nsajigwa hakuwahi hata kujaribiwa winga wa pembeni. Alicheza nafasi hiyo hiyo na akastaafu katika nafasi hiyo hiyo tu. Hakukuwa na mjanja wa kumbadili nafasi yake kwa ajili ya kumdumisha zaidi.

Hata Boniface Pawasa, hakuwahi kubadili nafasi yake.

Kwa nguvu alizokuwa nazo angeweza kuzeeka taratibu katika nafasi nyingine, hasa katika klabu nyingine ambayo haina ushindani mwingi.

Tatizo hatuna sayansi hii ya soka katika soka letu.

Leo Shiza Kichuya na Saimon Msuva ni mawinga. Wana kasi na umri unawaruhusu kuwa na kasi hiyo. Wanafunga kadiri wanavyojisikia.

Hata hivyo umri ukisogea hawataweza kufunga kwa kutumia kasi.

Kwa sayansi ya soka, itabidi wabadili aina yao ya uchezaji kwa ajili ya kuendelea kutamba. Wapo tayari kwa sayansi hii?

Ina maana kwa makocha wa kisasa, Msuva na Kichuya, itabidi wacheze washambuliaji wa kati na si mawinga tena kwa sababu kasi yao itakuwa imepungua.

Mchezaji ambaye aliweza kumudu kucheza kwa aina mbili alikuwa ni Ulimboka Mwakingwe.

Labda ndio maana aliweza kuongeza siku zake za kucheza soka.

Aliweza kucheza winga asilia, lakini pia aliweza kucheza eneo la katikati akiwa mshambuliaji wa nyuma ya mwenzake.

Wachezaji ambao wakiisha huwa hawawezi kurudi tena ni makipa tu.

Wengi hawawezi kuingizwa ndani ya uwanja.

Wengine ambao wakimalizika inakuwa ngumu kucheza katika nafasi nyingine ni washambuliaji wa kati.

Bahati nzuri ilikwenda kwa Zamoyoni Mogella.

Alikuwa anafunga sana na alikuwa na uwezo mkubwa wa kucheza mshambuliaji wa kati. Uwezo ulipoanza kupungua akawa mchezeshaji na wale wanazi wa Yanga wakampachika jina la DHL. Yaani msambaza vifurushi.

Wachezaji wengi wa Tanzania wamefia katika nafasi moja tu ambayo iliwatambulisha katika soka.

Wakati mwingine ndio maana tunasema tunahitaji kuanzisha soka la kisayansi zaidi katika nchi hii kwa kufuata misingi ambayo inafuatwa na watu wengine.