Yanga mamilionea

Muktasari:

Kuanzia mwaka 2016 hadi sasa, Yanga na KCCA ndio timu pekee kutoka ukanda huu unaoundwa na nchi za Sudan, Sudan Kusini, Eritrea, Ethiopia, Somalia, Djibouti, Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda zilizofanikiwa kufuzu hatua ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika na kuzipiga bao timu zenye majina makubwa na zinazoendeshwa kwa bajeti kubwa kama; Al Hilal, El Merreikh, Al Al-Ahly Shendi na Al-Hilal Al-Ubayyid.

MASTAA wa Yanga waliweka ahadi kuwa watapambana kuhakikisha wanasonga mbele kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, na sasa wameungana na KCCA ya Uganda kuweka historia kwenye michuano hiyo. Yanga na KCCA zimekuwa klabu pekee kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kufanya vizuri katika mashindano ya Afrika kwa ngazi za klabu kuliko zingine katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Kuanzia mwaka 2016 hadi sasa, Yanga na KCCA ndio timu pekee kutoka ukanda huu unaoundwa na nchi za Sudan, Sudan Kusini, Eritrea, Ethiopia, Somalia, Djibouti, Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda zilizofanikiwa kufuzu hatua ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika na kuzipiga bao timu zenye majina makubwa na zinazoendeshwa kwa bajeti kubwa kama; Al Hilal, El Merreikh, Al Al-Ahly Shendi na Al-Hilal Al-Ubayyid.

Mwaka 2016, Yanga ilifuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho baada ya kuitupa nje timu ya Sagrada Esperanca ya Angola kabla ya kurudia tena ubabe huo mwaka huu, baada ya kuiondosha Welayta Dicha ya Ethiopia katika hatua ya mtoano ya mashindano hayo.

Mchezo wajana, Yanga imefuzu hatua ya makundi licha ya kufungwa bao 1-0 ugenini dhidi ya Welaytta Dicha kwenye mechi iliyochezwa jana kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Awassa nchini hapa, kwani imewaondoa Wahabeshi hao kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1 ikinufaika na matokeo ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 kwenye mchezo wa kwanza uliofanyika kwenye Dar es Salaam siku 12 zilizopita. Hiyo ndiyo raha ya uwanja wa nyumbani.

Sahau kuhusu rekodi hiyo, baada ya kufuzu hatua hiyo, Yanga imejihakikishia fedha ya maana kutoka kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ambalo hutoa kitita cha Dola 275,000 (zaidi ya Sh 600 milioni) kwa kila timu inayofuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika. Pia Yanga italamba Sh250mil nyingine kutoka kwa wadhamini wao, SportPesa kama bonasi.

Hata hivyo, mafanikio Yanga haikupata mafanikio hayo kirahisi kwani imelazimika kufanya kazi kubwa ya nje na ndani ya uwanja ambayo pengine wawakilishi hao wa Tanzania wangeidharau Dicha hatua hiyo ya makundi wangeisikia kwenye bomba.

Nje ya Uwanja Yanga chini ya jopo la viongozi imara waliokuwemo kwenye msafara wake huku Ethiopia walitegua mitego kadhaa ambayo wenyeji waliiandaa ili kuwavuruga akili wawakilishi hao wa Tanzania, lakini kutokana na uimara wa vigogo hao wakiwemo Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Athuman Nyamlani, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Lameck Nyambaya, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili na Mashindano, Hussein Nyika na Katibu wake Samule Lukumay, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Salum Mkemi na Mkuu wa Idara ya Masoko na wanachama ya Yanga, Omary Kaya waliipangua.

Miongoni mwa mitego hiyo ni kupewa basi lisilokidhi viwango kwa ajili ya kuwasafirisha umbali mrefu kuja Awassa ambako, mechi hiyo ilichezwa pamoja na mbinu nyingine kibao za kuwavuruga kisaikolojia wachezaji.

Ndani ya uwanja, licha ya Yanga kupoteza kwa bao hilo la mapema ambalo lilifungwa na mshambuliaji Mtogo, Arafat Djako ambaye aliuwahi mpira wa kona ulioshindwa kuokolewa na Kelvin Yondani, Yanga ilionyesha kiwango bora ambacho kiliwashangaza wageni ambao, waliamini mechi ingekuwa rahisi kwa upande wao.

Dicha ambao husifika kwa kutandaza soka safi pindi wanapokuwa nyumbani, walilazimika kugeuka watumwa kwa Yanga ambayo ilimiliki mpira kwa zaidi ya dakika 60 za mchezo, lakini kukosekana kwa umakini kwenye safu ya ushambuliaji kuliwaangusha wawakilishi hao wa Tanzania kushindwa kuweka rekodi ya kuibuka na ushindi mnono ugenini.

Kurejea kwa nyota watatu tegemeo wa kikosi cha kwanza, Kelvin Yondani, Obrey Chirwa na Papy Tshishimbi kuliifanya Yanga iwe imara zaidi na kucheza soka safi ambalo liliwaweka wenyeji kwenye presha kubwa katika muda mrefu.

Ikifahamu fika kwamba matokeo yoyote ya sare, ushindi au kufungwa mabao yasiyozidi mawili kungewafanya wafuzu kuingia hatua ya makundi ya mashindano hayo, Yanga ilianza mechi taratibu ikionekana kama mbinu ya kuwasoma wapinzani wao ambao, waliingia uwanjani kwa shauku ya kusaka mabao ya mapema ili kuzima ndoto za wawakilishi wa Tanzania.

Tofauti na mechi ya kwanza Tanzania, Dicha walianza mechi kwa kasi dakika za mwanzo wakionekana kusaka mabao ya haraka ili wamalize mechi mapema, lakini Yanga ilionekana kutulia na kuwasoma wapinzani wao mbinu ambayo baadaye ilizaa matunda licha ya kuruhusu bao la mapema ambalo wenyeji walipata.

Yanga ilihimili presha hiyo ya mwanzoni ya wenyeji na kuanzia dakika ya 30 ya mchezo, ilicheza vizuri hasa kwenye safu ya kiungo na kutengeneza nafasi mara kwa mara ambazo hata hivyo hazikutumiwa kuipatia mabao.

Miongoni mwa nafasi hizo ni zile zilizopotezwa na Obrey Chirwa, Papy Tshishimbi na Abdallah Shaibu ‘Ninja’ katika vipindi vyote viwili vya mechi na kuleta afueni kwa Dicha ambayo ilionekana kukata pumzi mapema.

Nafasi mojawapo ambayo ingeipa Yanga bao ni ile ya Tshishimbi katika dakika ya 39 ambaye alipoteza nafasi baada ya kubaki ana kwa ana akiwa anamtazama kipa wa Dicha na, alipiga shuti lililopaa baada ya kupokea pasi ya Yusuph Mhilu.

Lwandamina apiga simu

SAA chache tu kabla ya Yanga kuingia uwanjani kuwakabili Dicha, nahodha wa Yanga Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na msaidizi wake, Kelvin Yondani ‘Vidic’ wakiwa wametulia na wachezaji wenzao, ghafla bosi mmoja wa akaingia eneo hilo na kuwapa simu ili wazungumze. “Sikilizeni simu yenu hiyo”.

Walipopokea wakakutana na sauti nzito, ilikuwa ya kocha wao Mzambia George Lwandamina, ambaye aliwaambia maneno mafupi yaliyowapa morali kinoma.

Kisha Cannavaro akawasilisha ujumbe huo kwa wenzake, akisema Lwandamina amewataka kuwa majasiri uwanjani na kupambana kuhakikisha wanapata ushindi.

“Ametaka tuingie uwanjani tukiwa tumesahau matokeo ya mchezo wa awali hivyo, tutafute mabao ya haraka haraka kisha wakae na mpira na tusijaribu kucheza soka wanalotaka wapinzani wetu.”

Lakini, kingine ambacho kilionekana kuwavutia zaidi wachezaji ni taarifa kuwa, Lwandamina bado hajasaini mkataba wa kuinoa Zesco United, hivyo lolote linaweza kutokea. Beki aliyepokea simu hiyo ni manahodha wawili wa timu hiyo Nadir Haroub Cannavaro na msaidizi wake, Kelvin Yondani ambao ujumbe walioambiwa na Mzambia huyo ni kwamba wanatakiwa kuwa majasiri na kupambana katika mchezo wa jana na zaidi kocha huyo anafuatilia kila taarifa katika timu hiyo.

Kilichowachanganya zaidi mabeki hao ni kauli ya Lwandamina akiwaambia hajasaini Zesco ingawa wanamuhitaji, lakini yeye bado ni kocha wao na wakati wowote uongozi wa Yanga ukiweka mambo sawa na wanasheria wake anarudi kufanya kazi yake muhimu washinde. Ujumbe huo uliwaongezea mzuka wachezaji wa timu hiyo ambao katika kikao chao cha asubuhi jana waliwapa ujumbe huo wenzao ambao nao walionekana kufurahia. Mwanaspoti liliwasiliana na Lwandamina, na alikiri kuzungumza na wachezaji akiwatakia kila la kheri.