‘Wachezaji wa Simba tatizo stamina’

Zanzibar. Kocha wa Mlandege, Jaala Abdallah amekitazama kikosi cha Simba katika mechi ya kirafiki dhidi yao juzi na kulishauri benchi lale la ufundi chini ya Joseph Omog kuhakikisha wanaongeza stamina kwa wachezaji.

Ushauri huo umetolewa zikiwa zimebaki siku nne kabla ya mechi ya ngao ya hisani itakayozikutanisha Simba na Yanga kwenye Uwanja wa Taifa, Jumatano.

Kocha huyo wa Mlandege alisema iwapo wachezaji wa Simba watakuwa na stamina ya kutosha, watamudu kukabiliana na Yanga ambayo inaonekana ipo imekamilika kwenye eneo hilo kulinganisha na Simba.

"Kwa bahati nzuri tumecheza na timu zote mbili ambapo tulianza kufungwa na Yanga kisha tukatoka sare na Simba. Kiujumla timu zote mbili zina wachezaji wazuri na wazoefu lakini kinachowabeba Yanga na kuwaangusha Simba ni stamina.

Sisi Mlandege ilikuwa kazi rahisi kwetu kuwabana Simba kwa sababu tuligundua wachezaji wao hawana stamina ya kutosha hivyo sisi tulihakikisha tuko vizuri kwenye hilo eneo lakini kwa Yanga walituzidi kwa sababu stamina yao ilikuwa iko juu," alisema Jaala.

Jaala aliongeza kuwa pamoja na changamoto hiyo inayowakabili Simba, bado haitoshi kuwafanya Yanga wabwete kwani pambano baina ya timu hizo huwa halitabiriki.

"Ile ni mechi kubwa ambapo maandalizi yake hayawezi kuwa sawa na haya ya mechi za kirafiki. Lakini kingine ni kuwa wachezaji sio siku zote wanaamka vizuri, hivyo unaweza kuona kwenye mechi hiyo, stamina ya Yanga ikawa iko chini huku ya Simba ikiwa juu," aliongeza kocha huyo.

Kocha msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja alisema kuwa watahakikisha wanamaliza kasoro zote zinazojionyesha kwenye maandalizi yao.

"Tunapocheza mechi za kirafiki, lengo letu kubwa ni kuyaona makosa hivyo kinachofuata sasa ni kwenda kuyafanyia kazi," alisema Mayanja.