Simba yampa presha kocha mpya Yanga

Muktasari:

  • Nyasi za uwanja husika huwa zinawaka moto miamba hiyo ya Kariakoo, Dar es Salaam inapovaana katika mashindano mbalimbali.

Dar es Salaam.Mchezo wa watani wa jadi Simba na Yanga siku zote umekuwa na presha kubwa bila kujali ubora au udhaifu wa timu ya upande mmoja.

Nyasi za uwanja husika huwa zinawaka moto miamba hiyo ya Kariakoo, Dar es Salaam inapovaana katika mashindano mbalimbali.

Presha ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, imenogesha mchezo wa wababe hao ambao wanateremka uwanjani Jumapili wiki hii katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kwa mara ya kwanza msimu huu, Yanga itacheza mchezo huo bila ya aliyekuwa kocha mkuu George Lwandamina, aliyetimkia nyumbani kwao Zambia.

Mzambia huyo hatakuwepo kwenye benchi, hivyo jukumu la kusimamia mchezo huo lipo mikononi mwa wasaidizi wake Noel Mwandila na Shedrack Nsajigwa.

Lakini, mabosi wa klabu hiyo ‘wamechungulia’ na kuona kuwa mchezo huo ni muhimu kushinda ili kupunga pengo la pointi baina yao, hivyo wamemleta haraka kocha mpya Mwinyi Zahera.

Zahera alikuwa kwenye benchi la ufundi la timu ya Taifa ya DR Congo akiwa kocha msaidizi kabla ya juzi usiku kutua Dar es Salaam kibabe.

Hata hivyo, Zahera amekaa Dar es Salaam kwa saa chache tu baada ya kuwasili kwa kuwa jana asubuhi aliwahishwa Morogoro kujiunga na kambi ya Yanga.

Presha ya mchezo dhidi ya Simba imemuondoa Zahera Dar es Salaam kwenda kuungana na kambi kwa lengo la kuongeza nguvu katika benchi la ufundi.

Ingawa uwezekano wa Zahera kukaa kwenye benchi ni mdogo kutokana na utaratibu wa kupata kibali cha kufanya kazi nchini, lakini Yanga itamtumia kiaina.

Rekodi na uzoefu wake unaweza kuwa chachu ya kuisuka Yanga kukabiliana na watani wao wa jadi katika mchezo huo.

“Baada ya kocha kupata taarifa kwamba mchezo huo ni muhimu kwetu ameomba kwanza aungane na timu kambini na baada ya hapo ndipo mambo mengine yatafuata.

“Kwa sasa atatazama kikosi kwa muda, kuwajenga kisaikolojia wachezaji na kutoa ushauri wa kiufundi, lakini baada ya hapo ndipo kazi rasmi itaanza, “ kilisema chanzo cha habari kutoka Yanga.

Akizungumzia ujio wake, Zahera aliyekuwa akizungumza zaidi lugha ya Kifaransa kuliko Kiswahili, alisema anajua Simba ni timu kubwa Tanzania na Afrika.

“Kwa ufupi bado sijafanya mazungumzo na uongozi, kwanza nimepanga kuitazama timu nikiwa Morogoro nitakaa na Kamati ya Utendaji kufanya mazungumzo na kutia saini mkataba nikiwa huko,” alisema Zahera kwa ufupi.

Yaikimbiza Simba uwanjani

Yanga jana iliilazimisha Simba kuhama uwanja kutoka Highland kwenda Uwanja wa Jamhuri.

Simba ilikuwa ya kwanza kufanya mazoezi kwenye Uwanja Highland, lakini wamelazimika kutafuta mwingine baada ya kubaini Yanga ilikuwa imetangulia kulipa mapema.

Jana jioni Yanga ilianza mazoezi katika Uwanja wa Highland, huku Simba wakiendelea kujifua Uwanja wa Jamhuri.

Yanga imeendelea kujifua na baadhi ya wachezaji nyota waliokuwepo kwenye mazoezi ni washambuliaji Ibrahim Ajibu, Donald Ngoma.