Salum Shebe anavyopambana klabuni Al-Mudhaibi

Muktasari:

  • Tanzania inawezaji wengi wa Kimataifa wanaocheza soka ndani na nje ya Afrika, kila mchezaji kati yao amekuwa na stori ya namna yake mpaka kutoboa.

KUTUSUA sio kitu chepesi. Walio wengi ambao wametusua wamekuwa na stori tofauti huku nyingine zikiwa za maumivu mpaka kufikia vileleni mwa mahitaji yao ambayo walikuwa wakiyapigania.

Tanzania inawezaji wengi wa Kimataifa wanaocheza soka ndani na nje ya Afrika, kila mchezaji kati yao amekuwa na stori ya namna yake mpaka kutoboa.

Wapo ambao waliondoka nchini kwa kufuata utaratibu wa kawaida na wengine wamezamia na ilipobidi kufanya udanganyifu hawakusita kubadili uraia wao.

Mwanaspoti tutakuwa tunakuletea mikasa tofauti ya wachezaji wenye asili ya Tanzania kwenye jarida hili la Nje ya Bongo, walivyofanya mpaka kutusua kwa kuibukia kwenye mataifa ya watu na kucheza soka la kulipwa.

Leo tunaye kiungo wa Kitanzania, Salum Shebe mzaliwa wa Visiwazi, Zanzibar ambaye amesalia kama Mtanzania pekee anayecheza soka la kulipwa nchini Oman kwenye klabu ya Al-Mudhaibi.

Awali, Shebe alikuwa akitunishiana misuli na Watanzania wengine kama Daniel Lyanga aliyekuwa akiichezea Fanja na Elius Maguli ambaye alikuwa akiitumikia Dhofar kabla ya kuchana na timu hizo.

Shebe anasema kuwa alianzia soka lake Visiwani Zanzibar na alizichezea timu kadhaa za Ligi Kuu kabla ya kupata bahati ya kwenda kutafuta changamoto nyingine za soka nje ya nchi.

“Nimezichezea timu nyingi kidogo, kuna Tembo,JKU,Taifa Jang’ombe na Mafunzo, kuna kocha mmoja anaitwa Hafidh Badru alikuwa akifundisha mpira Uarabuni kwa sababu alikuwa akinifahamu hasa uwezo wangu hakusita kunisaidia,”

“Hapo nilikuwa nimechoshwa tayari na soka la Zenji, nilitamani sana tangu nikiwa mdogo kucheza nje,2011 alinipa mualiko baada ya kumsumbua sana.

“Sio kwamba mwaliko ule uliambatana na tiketi ya ndege kwenda kule, hapana ilitakiwa nijihudumie kwenye usafiri, sehemu ya kulala haikuwa inshu, wakati ninacheza mpira ndani nilikuwa nikiwekeza kiasi kidogo ambacho nilikuwa nikikipata kwa kipindi hicho,” anasema Shebe.

Kiungo huyo, anasema alifanya taratibu kwa haraka za kuhakikisha ninakwenda, Oman ili kutimiza malengo yake ya kucheza soka la kulipwa nje ya nchini.

“Kila kitu kikakamilika, haikuchukua muda nikasafiri na kupokelewa na mwenyeji wangu, Hafidhi ambaye alinifurahia sana, mara baada ya kufika alinitembeza ili kuona wenzetu walivyoweka kwenye soka .

“Ndio ni kweli niliona namna ambavyo wamewekeza lakini sikuona maajabu ya soka lao kwa maana ya vipaji ambavyo nilivifanyia ulinganisho na vile vya nyumbani Tanzania.

“Nilivyozoea mazingira tukaanza mipnago ya namna gani anaweza kunisaidia kwa kunitafutia sehemu ndogo ya kufanya majaribio ili uwe kama msingi kwangu kabla ya kwenda timu kubwa zaidi nchini humo,” anasema nyota huyo.

Hafidhi hakuwa mtu mdogo nchini Oman, wengi walimfahamu kwa sababu alikuwa kocha hivyo Shebe anadai ndiyo maana kulikuwa na wepesi wa kumpeleka Al Rustaq kufanya majaribio.

Kiu yake ya kutaka kucheza soka la kulipwa ilimsaidia kufanya vizuri kwenye majaribio hayo na kusajiliwa kwenye timu hiyo ambayo ilikuwa kishiriki madaraja ya nchini.

“Sikudumu kabisa Al Rustaq, nilicheza kwa msimu mmoja na ndipo Al-Mudhaibi SC iliponisajili kwa dau nono ambalo lilinisaidia kwa kiasi chake kutengeneza maisha ya wazazi wangu nyumbani.

“Nilijiunga na Al-Mudhaibi SC ambayo ilikuwa daraja la kwanza, msimu huo tulipambana kila mmoja kwa nafasi yake na hatimaye kuipandisha timu daraja,” anasema Shebe.

Al-Mudhaibi SC ambayo imepanda daraja msimu uliopita ilikuwa na wakati mgumu wa kupata matokeo ya ushindi, mwanzoni mwa msimu kabla ya hivi karibuni kukaa sawa na kuanza kufanya vizuri.

“Ugeni wetu Ligi Kuu Oman ulitufanya kuwa vibonde kwa muda, lakini tulipoizoea ligi tuliendelea na kasi yetu ya uchezaji kwa kupata matokeo ya ushindi kwenye michezo mfululizo,” anasema.

Kinachomfanya Shebe kujituma zaidi kila kukicha ni uwepo wa idadi ndogo ya wachezaji wa kigeni ambao wanatakiwa kucheza nchini humo na uhodari wake umemsaidia kumpa namba kikosi cha kwanza.