Poulsen kinda wa Tanzania anayesumbua RB Leipzig

Muktasari:

  • Katika kikosi cha Stars yupo supastaa Mbwana Samatta anayekipiga Genk ya Ubelgiji, Simon Msuva (Difaa), Abdi Banda (Baroka) halafu unakutana na sura mpya kabisa, Yussuf Poulsen.

HEBU vuta picha umekaa katika kiti ndani ya sebule yako kisha unawasha runinga ukiwa na kikombe cha kahawa mkononi, ukiangalia mechi ya Taifa Stars dhidi ya Zambia a.k.a Chipolopolo.

Katika kikosi cha Stars yupo supastaa Mbwana Samatta anayekipiga Genk ya Ubelgiji, Simon Msuva (Difaa), Abdi Banda (Baroka) halafu unakutana na sura mpya kabisa, Yussuf Poulsen.

Ndio! Nafahamu una kiu ya kumfahamu huyu Poulsen ni nani kwenye kikosi cha Taifa Stars, huyu ni straika matata wa RB Leipzig ya Ujerumani, ambaye anauwasha moto kwelikweli huko Bundesliga.

Mshambuliaji huyu ni Mtanzania na angeweza kuibeba Taifa Stars lakini amechukua uraia wa Denmark, na huu ni msimu wake wa kwanza kuichezea RB Leipzig inayoshika nafasi ya tatu kwenye msimamo akiwa amecheza michezo 38 na kufunga mabao matano huku akiasisti mengine tisa.

Kwenye idadi hiyo ya mechi 38, Yussuf amecheza mechi 27 za Bundesliga kati ya mechi 31 ambazo timu yake imecheza mpaka sasa na kwenye mechi hizo amefunga mabao manne na kutengeneza matatu.

Pia, amecheza michezo mitano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (Uefa) kati ya sita na kutengeneza bao moja kwenye hatua ya makundi ambapo, timu yake ilimaliza kwenye nafasi ya tatu kwenye Kundi G na kuangukia kwenye michuano ya Europa League.

Akiwa na Leipzig kwenye michuano ya Europa League alicheza michezo minne ukiwemo ule waliotolewa na Marseille kwa jumla ya mabao 6-3 kwenye hatua ya 16 bora.

Baba wa Yussuf ni Mtanzania na mwenyeji wa Mkoa wa Tanga, Shihe Yurary anayejishughulisha na biashara ya usafirishaji kati ya Afrika na Denmark wakati mama yake, Lene ni raia wa Denmark.

Kupitia biashara zake hizo, Shihe alikutana na Lene na kuanzisha uhusiano uliomleta duniani Yussfuf na hapo akaamua kuhamishia makazi yake jijini Copenhagen, Denmark.

Yussuf katika ukuaji wake alikuwa na mzuka mkubwa na soka, ambapo akiwa na miaka sita tu baba yake alifariki dunia kwa ugonjwa wa kansa, hivyo kulelewa na mama yake.

Kwa sasa ni staa mkubwa akishumbua kwenye Bundesliga na pia ameichezea Timu ya Taifa ya Denmark, ambako amechukua uraia wa nchi hiyo. Mpaka sasa Yussuf ameichezea Denmark mechi 24 tangu mwaka 2014 alipoitwa kikosini humo akiwa amefunga mabao matatu.

Hata hivyo, straika huyo bado ameonyesha mapenzi makubwa kwa Tanzania, ambapo amekuwa akisaidia shughuli mbalimbali za kijamii. Kwa sasa ametangaza kusaidia mamilioni ya shilingi kwa Kituo cha Mwandaliwa kilichopo Mbweni, ambacho kinahudumia watoto wasiojiweza.

Pia, amehamasisha watu wengine kukisaidia kituo hicho ili kuleta ustawi wa maisha ya watoto hao.