Modric awakaba koo Real Madrid

Muktasari:

La Gazzetta dello Sport linafichua kwamba Real Madrid wameshtuka baada ya kusikia kwamba Inter wanamhitaji staa huyo wa kimataifa wa Croatia na mwenyewe yupo tayari kutua Serie A.

MADRID, HISPANIA. KIUNGO fundi wa mpira, Luka Modric, anatarajia kukutana na mabosi wa Real Madrid leo Ijumaa kuzungumzia hatima yake kikosini humo baada ya Inter Milan kuonyesha nia ya kumhitaji.

La Gazzetta dello Sport linafichua kwamba Real Madrid wameshtuka baada ya kusikia kwamba Inter wanamhitaji staa huyo wa kimataifa wa Croatia na mwenyewe yupo tayari kutua Serie A.

Rais wa Real Madrid, Florentino Perez, ameamua kuyapuuza mazungumzo na mabosi wenzake wa Inter Milan na kilichopo kwa sasa ni kuhakikisha Modric anapewa mkataba mpya utakaomshuhudia mshahara wake ukienda juu zaidi.

Kwenye mkataba wa Modric, kuna kipengele kinachofichua kwamba timu itakayotaka kumsajili basi inapaswa kulipa Euro 750 milioni.

Mkataba wa sasa wa staa huyo utafika tamati mwaka 2020 na Modric analipwa Euro 8 milioni kwa mwaka, wakati Inter Milan wamempa ofa ya mkataba wa miaka minne wenye thamani ya Euro 10 milioni kwa mwaka.

Real Madrid sasa imekubali yaishe na itampa mshahara mkubwa Modric ili abaki wasimpoteze kama ilivyotokea kwa Cristiano Ronaldo, aliyetimkia Juventus. Mazungumzo baina ya Modric na wawakilishi wake pamoja na mabosi wa Los Blancos yatafanyika leo.