Mkwewe Kiba afunguka, haamini

Muktasari:

Kiba anafunga ndoa leo mjini hapa na mrembo Amina Khaleef huku shamrashamra zikirindima kila kona huku ukumbi wa Diamond Jubilee itakapofanyika sherehe hiyo ukipambwa kwa gharama ya Sh40 milioni.

AMSHA AMSHA ya harusi ya supastaa wa Bongo Flava, Ali Kiba imezidi kupamba moto mjini Mombasa, ambako upande wa mwanamke umekuwa bize kwelikweli.

Kiba anafunga ndoa leo mjini hapa na mrembo Amina Khaleef huku shamrashamra zikirindima kila kona huku ukumbi wa Diamond Jubilee itakapofanyika sherehe hiyo ukipambwa kwa gharama ya Sh40 milioni.

Mwanaspoti ambayo imekuwa mstari wa mbele kuchimba kila kinachofanyika kwenye harusi hiyo kwa ajili ya kuhabarisha wasomaji wake, limezamia hadi ndani ya ukumbi huo kuangalia maandalizi.

“Zaidi ya pesa hizo zimelipwa kwani tunapamba ukumbi na steji ambayo itatumika. Ukumbi huu utakuwepo na viyoyozi, maua ya waridi pamoja na mapambo mengine mengi ambayo yamelipwa,” alisema msimamizi wa matayarisho hayo ambaye hakutaka kutajwa kwa sababu ya usiri wa harusi hiyo.

Kwa mujibu wa wamiliki wa Ukumbi wa Diamond Jubilee mjini Mombasa, gharama za kukodi ni kati ya Sh 1.2 milioni hado 1.4 milioni kwa siku, ambapo jana ilikuwa siku ya pili ukumbi huo ukiendelea kupambwa. Hii inamaanisha kwamba, Kiba amekodisha ukumbi huo unaochukua watu 500 kwa wakati mmoja, kwa zaidi ya siku mbili hivyo, gharama kupanda zaidi.

Mwanaspoti limezungumza na mama mzazi wa bi harusi, Asma Said ambaye kwanza ameonyesha kutoamini kwa binti yake kuolewa na Kiba, akisema ni bahati ya kipekee.

Pia, amesema kuwa kwa wiki nzima sasa nyumbani kwake kuwamekuwa na hekaheka za kila aina ili kuhakikisha harusi hiyo inafana. Habari ambazo Mwanaspoti inazo na zilizothibitishwa na Bi Asma ni kwamba, Kiba na familia yake wamekwishatua mjini Mombasa na wameweka kambi kwenye hoteli ya English Point Marina, ambako ni jirani na nyumbani kwa Bi harusi mtarajiwa, eneo la Kongowea.

“Ni bahati iliyoje, kijana ametoka Tanzania na kuja kuoa Kenya, sikujua kama mtoto wangu ataolewa na Ali Kiba, lakini Mungu ndio aliyepanga hili kutokea namshukuru sana,” alisema Bi Asma.

Kwa mujibu wa ratiba kamili ya harusi hiyo, Kiba amefunga ndoa alfajiri ya leo katika Msikiti wa Ummul Kulthum uliopo eneo la Kizingo.

Msikiti huo umejengwa na familia ya Gavana wa Mombasa, Hassan Joho ambaye ni rafiki mkubwa wa Ali Kiba na atakuwepo kwenye sherehe hiyo mwanzo mwisho huku akiwa ndiye aliyefanikisha kwa kiasi kikubwa.

Mpango mzima utakuwa jioni, ambapo sherehe ya kukata na shoka itafanyika Ukumbi wa Diamond Jibilee huku Joho akiongoza kundi kubwa la wageni waalikwa akiwemo Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete.

Mbali na wageni hao mashuhuri, pia kutakuwepo na wasanii mbalimbali wa Kenya na Tanzania, akiwemo swahiba wa Kiba, Ommy Dimpoz. Shughuli haitaishia hapo tu, kwani hapa nyumbani kutafanyika nyingine hapo Aprili 29, ambako wageni kibao watahudhuria. Kumbuka harusi hii itakwenda mubashara kupitia Azam Tv.