Mbao FC moto umewaka

Muktasari:

Timu hiyo ambayo ilipanda Ligi Kuu msimu uliopita na kuonyesha ushindani wa hali ya juu kiasi cha kumezewa na mate na klabu kubwa kama Simba, Yanga na Azam FC, imekuwa tofauti na msimu huu na inaonekana kupwaya kupita maelezo.

MAMBO si shwari ndani ya klabu ya Mbao FC kwa sasa, inapoelekea tunaweza kusema mengine kama juhudi binafsi na zenye busara hazitatumika kuinusuru timu hiyo isishuke daraja.

Timu hiyo ambayo ilipanda Ligi Kuu msimu uliopita na kuonyesha ushindani wa hali ya juu kiasi cha kumezewa na mate na klabu kubwa kama Simba, Yanga na Azam FC, imekuwa tofauti na msimu huu na inaonekana kupwaya kupita maelezo.

Mashabiki na wadau wa soka jijini hapa wameanza kuikatia tamaa na kuihusisha na moja ya timu zinazoweza kushuka daraja msimu huu.

Mbao hadi sasa imecheza mechi 25 na kukaa nafasi ya 12 katika msimamo wa Ligi Kuu, ambapo imebakisha michezo mitano na timu za Mwadui, Yanga na Stand United (Ugenini), Ndanda na Ruvu Shooting itakazocheza nyumbani.

Kutokana na hali hiyo, Mwanaspoti linakuletea mambo kadhaa, ambayo yanaifanya timu hiyo kutokuwa katika ubora iliouonyesha katika msimu uliopita.

Kukamia mechi kubwa

Hii imeiathiri sana Mbao kwa kukamia mechi kubwa hasa za Simba,Yanga na Azam FC tofauti na inapokuwa ikicheza mechi na timu za kawaida jambo ambalo limeifanya kuwa katika wakati mgumu.

Viongozi, benchi la ufundi na wachezaji imekuwa ikitumia nguvu kubwa inapokutana na aidha Simba au Yanga, tofauti na inavyojipanga kuzikabili timu nyingine kama Lipuli, Stand United na Kagera Sugar.

Kitendo hicho kimeonekana wazi kuidhohofisha sana Mbao na kujikuta ikipata matokeo mabovu inapokutana na timu ndogo na kusahau kama timu inapaswa kujipanga na timu zote.

Pia, kitendo hicho, kimezifanya timu nyingine kukaza buti pindi zinapokutana nayo zikiamini nayo ni timu kubwa kumbe bado ni changa tu Ligi Kuu.

Kuondokewa na nyota wake

Baada ya msimu wa 2016/17 kumalizika na baadhi ya wachezaji waliokuwa moto kikosini humo kuondoka, Mbao FC haikufanya usajili mkubwa wa kuziba nafasi zao.

Tulishuhudia wachezaji kama Asante Kwasi, Salmin Hoza, Jamal Mwambeleko, Benedict Haule, Pius Buswita na Emanuel Mseja wakitimkia kwenye klabu za Simba, Yanga na Azam.

Benchi la Ufundi lenye dhamana ya kupendekeza na kusajili wachezaji wenye ushindani, halikufanya hivyo badala yake likatafuta wachezaji wa kawaida, ambao kwa sasa inaonekana wazi wameshindwa kuhimili mikiki mikiki ya Ligi kuu.

Mbao ambayo msimu uliopita iling’ara hadi kufika hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho (FA), msimu huu iliaga mashindano hayo katika hatua ya 16 bora kwa kuondoshwa na Njombe Mji.

Mfumo wa Timu

Mbao FC ina tofauti na msimu uliopita, kwa sasa imekuwa na mfumo wa kupaki basi, jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa kuwa na ukame wa mabao, huku ikiruhusu mabao mengi.

Katika mechi nyingi za msimu huu Mbao FC imekuwa ikijilinda zaidi, kuliko kushambulia, suala ambalo limeiweka kwenye hatihati ya kushuka daraja kutokana na kukosa ushindi.

Timu ambayo ina matokeo mabaya, haiwezi kucheza kwa mfumo wa kuzuia, hapo ilipaswa kushambulia zaidi na kusaka ushindi ili kujinasua nafasi za chini.

Pia, falsafa ya Kocha Mrundi, Ettiene Ndayiragije ya kutokuwa na kikosi kamili cha kwanza, nayo imechangia kuwa na mwenendo mbovu. Mara kadhaa wachezaji wengine wamekuwa wakicheza bila kuwa katika kiwango bora. Ilishuhudiwa katika mchezo dhidi ya Lipuli, nyota wake ambao wangeweza kupambana kutafuta ushindi,waliwekwa benchi bila sababu na kuwapa nafasi chipukizi.

Tuliwaona kipa Mussa Mussa, Kelvin Kijiri, Ayoub Lipart na wengine wakianza, huku kina Yvan Rugumandiye, Vincent Philipo, David Mwasa, Boniface Maganga na Ibrahim Njohole wakiachwa Benchi.

Mabadiliko benchi la ufundi

Ni kama vile Mbao imefanya mabadiliko katika benchi lake la ufundi kwa kumpa nafasi Kocha Msaidizi wa Taifa Stars, Novatus Fulgence na Jumapili iliyopita ndiye aliyesimamia mechi yao dhidi ya Majimaji.

Kuongezeka kwa kocha huyo wengi walitarajia Mbao ingeweza kupata pointi tatu ili kujiweka nafasi nzuri katika msimamo wa Ligi Kuu katika vita ya kukwepa janga la kushuka daraja lakini mambo hayakuwa tofauti sana kwani matokeo ya mwisho yalikuwa 2-2. Baada ya kocha huyo kutua, aliyekuwa Kocha Mkuu, Ndayiragije hajaonekana tena kwenye benchi huku taarifa za chini zikisema amerejea kwao Burundi baada ya kushindwana na viongozi wa Mbao.

Kocha mpya, Flugence anasema: “Nitaanzia pale nilipoikuta timu, hasa katika kurekebisha makosa ambayo yanaonekana wazi, niombe zaidi ushirikiano kwa wadau na wenzangu katika benchi la ufundi.”

Uongozi wafafanua

Mwenyekiti wa klabu hiyo, Solly Njashi anasema bado wana mkataba na Ndayirageje na kitendo cha kuongeza nguvu kwenye benchi la ufundi si kama wamemfukuza.

Njashi anasema wameongeza nguvu kutokana hali ya timu ilivyo, kwani lengo ni kuhakikisha Mbao inabaki Ligi Kuu tena katika nafasi nzuri.

“Tumeona kuongeza nguvu kwenye benchi la ufundi kunaweza kusaidia kuinusuru timu kubaki Ligi Kuu, bado Ndayiragije ni kocha wetu ambaye tuna mkataba naye na hatujamfukuza,” anafafanua Njashi.

Kiongozi huyo anaongeza kuwa licha ya kwamba timu haipo sehemu nzuri, lakini menejimenti yao inaendelea kupambana kutimiza wajibu wake na kuiwezesha kumaliza ligi vyema.

“Mafanikio pia ni mengi kwa Mbao ukilinganisha na muda ambao imeanza kucheza Ligi Kuu,lakini hata changamoto zipo, hivyo tunajitahidi kupambana nazo,”anasema Njashi. Pia anasisitiza kuwa Mbao haina mgogoro wowote kwani kila mmoja anawajibika kulingana na nafasi yake, hivyo anawaomba wadau wa soka jijini Mwanza kuungana ili kuiletea timu mafanikio.

Kuhusu kukamia mechi za timu kubwa, mwenyekiti huyo anasema michezo yote kwao ni sawa, isipokuwa wachezaji wenyewe hufanya hivyo ili kutafuta soko na kusisitiza maandalizi kama viongozi huyafanya kwa timu zote.

“Sisi maandalizi huwa tunayafanya kwa timu zote, isipokuwa wachezaji wakisikia wanacheza na Simba au Yanga huongeza morari na nafikiri ni kutafuta soko,”anasema Njashi.

Mashabiki wanena

Mashabiki wa klabu hiyo wanasema hawana ubaya wowote na kocha Ndayiragije, isipokuwa wanachohitaji ni ushindi wa timu yao na si vingine.

Shabiki Paschal Benard anasema wanaumizwa sana na matokeo yasiyoridhisha, hivyo hawawezi kuendelea na kocha ambaye hawapi furaha uwanjani. “Tunachohitaji ni ushindi tu, hatuna shida nyingine, kama kuna makosa yeye kama kocha ayafanyie kazi, siyo kila siku tunatoka tumenuna,” anasema.