Kumbe Kane anajua kama anachekwa kitaa

Muktasari:

Kane alipewa bao lililofungwa na Christian Eriksen baada ya kudai mpira ulimgusa kwenye bega kabla ya kutinga wavuni katika mechi yao ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Stoke City kwenye Ligi Kuu England.

LONDON,ENGLAND

STRAIKA Harry Kane amesema hajali kitu kuhusu watu kumsemasema tangu aliposhinda rufaa yake na kupewa bao kwenye Ligi Kuu England.

Kane alipewa bao lililofungwa na Christian Eriksen baada ya kudai mpira ulimgusa kwenye bega kabla ya kutinga wavuni katika mechi yao ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Stoke City kwenye Ligi Kuu England.

Kane alikata rufaa ili apate bao hilo limsaidie katika kumfukuzia Mohamed Salah kwenye mbio za Kiatu cha Dhahabu ambapo kwa sasa amefunga mabao 26 huku mpinzani wake akiwa na mabao 30.

Tangu tukio hilo lilipofanyika, Kane amekuwa kituko kwenye mitandao ya kijamii kwa mashabiki wakimdhihaki, huku mwenyewe akidai jambo hilo wala halimsumbui kichwa chake.

“Watu wanasema sana na kufanya utani kwenye mitandao ya kijamii. Lakini, kazi yangu nikuwa uwanjani na kujaribu kufanya kazi yangu kwa nguvu zote,” alisema.

“Hayo mambo ni sehemu tu ya mchezo katika miaka ya karibuni. Watu wanaweza kutoa maoni yao, mimi sijali kitu. Kuna watu wanacheka, lakini mimi nimeelekea akili katika kazi yangu. Salah anafanya vizuri na tumebakiza mechi nne subiri tuone itakavyokuwa.”

Kane, aliibuka kinara wa mabao katika misimu mwili mfulululizo iliyopita, huku Salah akiwa mbele kwa mabao manne kwenye kinyang’anyiro cha kuwania Kiatu cha Dhahabu.