Kitenge kiboko ya Kindoki alilia mpira wake

Muktasari:

  • Ni utamaduni uliozoeleka duniani kote mchezaji akifunga mabao matatu basi atapewa ule mpira uliotumika katika mchezo husika

Dar es Salaam. Mshambuliaji Stand United, Mrundi Alex Kitenge bado analilia mpira wake alionyang'anywa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya kumtungua mabao matatu kipa wa Yanga, Claus Kindoki.

Kitenge alisema baada ya kupewa mpira ule na kupiga nao picha viongozi wa TFF walimuomba arudishe kwa madai wana mipira michache, hivyo watamtafutia mwingine.

Mrundi huyo alisema baada ya tukio hilo aliwauliza kwa kupoteza haki yake na utakuwa kumbukumbu ya kuifunga timu aliyokuwa anaisikia ndio nembo ya kufanya vizuri Tanzania.

"Najisikia vibaya kwa sababu mpira huo ni haki yangu na sijui ni lini kocha ataenda kunifuatia, kwani nahitaji uwekwe kwenye rekodi ya kazi zangu ninazoendelea kuzifanya katika soka la Tanzania,” alisema Kitenge.

Anaongeza kabla ya mechi alishaambiwa mapema kwamba ndani ya kikosi cha Yanga kuna beki anaitwa Kelvin Yondani ambaye hapendi kupitwa na washambuliaji, jambo lililomfanya ajihami na aingie uwanjani akiwa amejiapiza.

"Kitu cha kwanza nilipoingia uwanjani, nilimsoma Yondan kwa dakika 10 nikajua ubora na mapungufu yake, baada ya kufanikiwa yote hayo nikaanza lengo la pili ambalo lilikuwa ni kufunga, nilitamani iwe zaidi ya mabao matatu ila muda haukuwa rafiki kwangu," alisema.   

Alipoulizwa kocha msaidizi wa timu hiyo, Athuman Bilali 'Bilo' juu ya jambo hilo alijibu kuwa "TFF watuomba kwamba mpira walioutoa wanaenda kuutumia kwenye mashindano ambao anatakiwa abaki nao moja kwa moja tuende kuuchukua.

"Leo ndio tunataka kwenda kuufuata mpira wake, hakuna tatizo lolote baina yetu na TFF mchezaji atapatiwa haki yake bila tatizo," alisema Bilo.

Ofisa habari wa TFF, Cliford Mario Ndimbo alisema Kitenge aliambiwa aende kuchukua mpira wake makao makuu wa Shirikisho hilo, Karume jijini Dar es Salaam.

"Baada ya mechi tulimkabidhi mpira kama 'demo' kwani mpira ule si ile inayotumika katika Ligi, ule ni wa CAF (Shirikisho la soka la Afrika) ambayo inatumika kwenye mashindano ya kimataifa na ndiyo wanayoitumia Taifa Stars siku ile ililetwa uwanjani kimakosa kwani aliyebeba alisahau ile ya Ligi na kubeba hiyo," alisema Ndimbo.