Kenya yatinga fainali Hong Kong 7s

Nairobi.  Kenya imefanikiwa kutinga hatua ya fainali ya Kombe la Dunia Raga, kwenye msururu Hong Kong 7s, baada ya kuwalaza wapinzani wao wa jadi, timu ya New Zealand 21-12.
Kwa matokeo hayo, Kenya maarufu Shujaa 7s, imejikatia tiketi ya kulipiza kisasi dhidi ya Fiji huku pia wakiweka rekodi ya kufuzu fainali mara mbili mfululizo kwenye misururu hiyo ndani ya msimu mmoja.
Cheko la Shujaa 7s lilianza baada ya Collins Injera kuvuka mstari mara mbili huku Willy Ambaka akiongeza la tatu na kuipatia Kenya sababu ya kuooza machungu dhidi ya Fiji watakapokutana nao tena.
Katika fainali ya Vancouver 7s, Shujaa inayonolewa na Innocent Simiyu iliangukia pua mbele ya Fiji inayoshikilia nafasi ya kwanza kwa ubora duniani, baada ya kukubali kichapo cha 31-12.
Injera alifikisha 'try' ya 254 katika misururu ya mashindano ya Kombe la Dunia la Raga maarufu kama HSBC World Rugby Sevens Series baada ya kufungia Kenya  mbili kabla Willy Ambaka hajapiga la tatu.
Kwa upande wao, New Zealand maarufu kama All Blacks, walijipatia 'tries' zao mbili kupitia kwa Rocky Khan aliyepokea pasi ya Amanaki Nicole ambaye alikuwa moto wa kuotea mbali katika mchezo huo wa nusu fainali ya pili.
Juhudi za New Zealand kutaka kubadili upepo zikiwa zimesalia dakika chache mchezo umalizike ziliishia kuwapa pointi tano tu kutokana na kazi nzuri ya Jona Nareki. Hadi mwisho wa mechi matokeo yalisalia 21-12 na Kenya wakafuzu.
Katika mechi ya nusu fainali ya kwanza, Fiji walikatia tiketi baada ya kuwapiga wawakilishi wengine kutoka Afrika, timu ya Afrika Kusini 26-24.