Huu ndio mzuka wa Hilal Chemelil Sugar

Muktasari:

  • Tayari winga huyo ameichezea, Chemelil Sugar mechi nane na kupachika mabao manne na kuasisti mengine mawili kwa timu yake tangu atue mwanzoni mwa mwaka huu.

WINGA wa Kitanzania anayekipiga Tusker FC ya Kenya, Abdul Hilal ambaye kwa sasa ametolewa kwa mkopo Chemelil Sugar, ametoboa siri iliyompa mzuka hadi kurejea kwenye makali yake ya kupachika mabao.

Tayari winga huyo ameichezea, Chemelil Sugar mechi nane na kupachika mabao manne na kuasisti mengine mawili kwa timu yake tangu atue mwanzoni mwa mwaka huu.

“Kiwango changu kinarejea kwa kasi, pale Tusker hawakuwa wakiniamini vya kutosha na kunipa nafasi, lakini hilo lilikuwa tatizo huku ndio nimeuwasha moto kisawasawa.

“Tangu nifike hapa nimeingia moja kwa moja kikosini na kocha ananiamini ndio sababu ya kurejea kwenye makali yangu,” alisema Hilal.

Hilal, ambaye aliwahi kuichezea African Lyon kabla ya kwenda Kenya kutafuta changamoto mpya, amesaini mkataba wa awali wa kujiunga na Zanaco ya Zambia na anategemea rasmi kujiunga na timu hiyo mwishoni mwa msimu.

“Sina mpango hata kama Tusker ikihitaji huduma yangu kwa kuniomba niongeze mkataba, siko tayari kwa sababu nakwenda kukipiga Zambia na baada ya hapo ni Afrika Kusini,” alisema winga huyo.