Chelsea hakuna kulala kwa Man United FA

Muktasari:

  • Chelsea inatarajiwa kumenyana na Manchester United katika mchezo wa fainali baada ya kuilaza Southampton ‘Watakatifu’.

London, England. Nahodha wa Chelsea Gary Cahill, amesema wanataka ubingwa wa Kombe la FA ili kupunguza presha msimu huu.

Chelsea inatarajiwa kumenyana na Manchester United katika mchezo wa fainali baada ya kuilaza Southampton ‘Watakatifu’.

Libero huyo alisema Chelsea inatakiwa kutwaa ubingwa baada ya kupokwa Kombe la Ligi Kuu England na Manchester City.

Alisema baada ya kupoteza ubingwa wa England, jukumu lao ni kuifunga Man United katika mchezo wa fainali.

Tangu kuanza msimu huu Chelsea imeshindwa kutamba chini ya kocha Mtaliano Antonio Conte licha ya kuipa ubingwa msimu uliopita.

Cahill alisema endapo Chelsea itakuwa mabingwa, itarejesha morali ya kufanya vyema katika Ligi Kuu.

“Ligi Kuu haitabiriki. Malengo yalikuwa kushinda na kutwaa ubingwa, lakini msimu huu hali imekuwa ngumu kwetu,”alisema Cahill.

Mchezaji huyo alisema Kombe la FA lina heshima kubwa na mashabiki wana matarajio Chelsea itawapoza machungu kwa kutwaa ubingwa.