Benchi lampoteza Edo Kagera Sugar

Mwanza. Mshambuliaji wa Kagera Sugar, Edward Christopher ‘Edo’ amesema kukosa namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza ndiyo sababu ya kutokuwa miongoni mwa wafungaji bora wa Ligi Kuu msimu huu.

Safu ya Ushambuliaji ya Kagera Sugar msimu huu inaundwa na   Pastory Athanas, Atupile Green, Themi Felix, Selemani Magoma na Venance Ludovic.

Hadi sasa mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba na Toto Africans amefungia mabao matatu kwa timu yake hiyo inayoshika nafasi ya 11 ikiwa na pointi 22 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi anaongoza kwa kufunga mabao 16, akifutiwa na Obrey Chirwa wa Yanga aliyefunga 12 na John Bocco (Simba) akitupia mabao 10.

Edo alisema malengo yake yalikuwa ni kukifukuzia kiatu cha mfungaji bora, lakini kutokana na kukosa namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza kimemtibulia mipango.

Alisema mara nyingi amekuwa akitokea benchi kutokana na ushindani wa namba ulivyo kikosini pamoja na mipango ya Kocha kupanga nani acheze kulingana na mchezo husika.

“Ushindani wa namba umekuwa mkali, lakini hata mipango ya benchi la ufundi ndilo linajua nani acheze kwenye mchezo husika, kikubwa ni kuendelea kupambana,”alisema Edo.

Aliongeza kuwa hawezi kukata tamaa na badala yake atahakikisha mazoezini anafanya vizuri ili kumshawishi kocha Mecky Maxime aweze kumpanga kikosi cha kwanza mechi zilizobaki.