cheki Man Utd waanza tizi mdogomdogo

Muktasari:

  • Kikosi hicho kimesafiri kwa maili 5,200 kutoka England kwenda California, Marekani kwa ajili ya kufanya mazoezi makali, huku ikimkosa staa wake Alexis Sanchez baada ya kuzuiwa kuingia Marekani.

MANCHESTER United imeanza kujifua kujiandaa na msimu mpya japo si kikosi kizima kutokana na wakali wengine waliokuwa kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018 wakipewa likizo ya wiku tatu. Kocha Jose Mourinho anataka mastaa wake kuwa kwenye ubora mkubwa kabla ya kuanza kwa msimu mpya kwenye Ligi Kuu England.

Kikosi hicho kimesafiri kwa maili 5,200 kutoka England kwenda California, Marekani kwa ajili ya kufanya mazoezi makali, huku ikimkosa staa wake Alexis Sanchez baada ya kuzuiwa kuingia Marekani.

Kutokana na hilo, Sanchez sasa amebaki Carrington na kufanya mazoezi kivyake. Supastaa huyo wa Chile, amekosa visa ya kuingia Marekani baada ya kukutwa na hatia ya kukwepa kodi huko Hispania, wakati alipokuwa akiichezea Barcelona. Fowadi huyo alikwepa jela baada ya kulipa Pauni 890,000 thamani ya kodi na fidia nyingine baada ya kukubali makosa ambayo yangemfanya awekwe jela kwa miezi 16. Kutokana na hilo, limekuwa kikwazo kwake cha kupata ruhusa ya kuingia Marekani.

Huko Marekani, mastaa wa Man United wanajifua katika viwanja vya Chuo Kikuu cha California huko Los Angeles. Luke Shaw, Andreas Pereira, Antonio Valencia, Anthony Martial na Chris Smalling walionekana wakifanya mazoezi ya kupasha misuli yao moto kujiweka sawa baada ya safari ya saa kadhaa hewani. Eneo wanalofanya mazoezi Man United lina vifaa vya kutosha na hali ya hewa ni nzuri kabisa, huku ikiwa ni mahali ambako mastaa kibao wa Hollywood wamekuwa wakipenda kwenda kutembelea.

Kuanzia Ijumaa hii, Man United wataanza kasheshe la kutambua nguvu ya kikosi chao wakati watakapocheza na Club America, San Jose Earthquakes, AC Milan, Liverpool na Real Madrid ambao ni mfululizo wa mechi za kirafiki iliyopanga kucheza kwenye ziara yao hiyo kabla ya kurudi England kumalizia mambo mengi kusubiria msimu mpya kuanza.

Ukimweka kando Sanchez, mastaa wengine wa Man United ambao hawapo kwenye ziara hiyo ya Marekani ni Paul Pogba, anayeshangilia ubingwa wa dunia na Ufaransa huko kwao, wakati wengine ni Marcus Rashford, Jesse Lingard, Romelu Lukaku, Marouane Fellaini, Victor Lindelof, David De Gea na kiungo mpya, Mbrazili Fred.

Wachezaji wapya, Diogo Dalot na Lee Grant wamekwenda, lakini kiraka Daley Blind ameachwa kutokana na kuwa na mpango wa kutaka kurudi zake Ajax kwa ada ya Pauni 18.1 milioni.