West Ham walitafakari vyema kumwajiri Moyes?

Tuesday November 14 2017

 

ISRAEL SARIA LONDON. UPO msemo usemao, mmoja akiumwa na nyoka basi akiona ujani anaogopa na mwingine unasema ukiona wenzako wananyolewa basi tia maji. Yote hii ni kwa ajili ya kuwajenga wana wa ulimwengu huu katika mienendo yao.

Wanapofikiria au kuchukua uamuzi wasifanye hivyo tu kama jiwe linavyodondoka bali baada ya tafakari kubwa, pia kutazama na kujifunza kwa yalitotokea kwa wengine. Haya yalitarajiwa sana kwa klabu kadhaa za Ligi Kuu England (EPL) na hata kwa Bayern Munich, Ujerumani waliokumbwa na mkasa kama huu.

EPL kulikuwa kunafuka baada ya timuatimua ya makocha msimu huu wa 2017/18, ukianza na Frank de Boer wa Crystal Palace; Craig Shakespeare wa Leicester; Ronald Koeaman wa Everton na Slaven Bilic. Ni uzibaji pengo wa huyu wa mwisho nalenga kujadili leo kwa misingi niliyotanguliza awali.

Bilic alifanya vyema alipoanza kazi 2015 lakini kadiri muda ulivyokwenda timu ikaonekana kutofanya vyema, licha ya wachezaji ni kana kwamba walikuwa wale wale. Alishawaimarisha vyema na alianza kuogopewa na hata timu zile sita pale juu. Mafanikio hayakudumu, klabu wakaelekea kwenye eneo la kushuka daraja na wenye timu hawakumkawiza wakamwelekeza pa kutokea.

Sasa ameletwa David Moyes. Najiuliza sana na kuona kuwa West Ham hawakufanya utafiti wa kutosha kabla ya kuchukua uamuzi wa kumpa mikoba Moyes.

Wapo wanaohoji iwapo jamaa waliompa ajira walizungumza na mmiliki wa Sunderland, Mmarekani Ellis short kupata taarifa ya ndani juu ya mambo yalivyokuwa Sunderland alipomchukua Mscotland huyu ili awaepushe na kadhia ya kushuka daraja.

Aliikuta Sunderland inafanya vibaya; akadai ana mbinu za kuwatuliza na kuwapeleka kwenye mwelekeo wa kushinda mechi, lakini haikuwa wakashuka hadi walipogota hapo Championship kisha akaondoka zake.

Moyes anadaiwa kutopendwa na wachezaji wake mwenyewe, wakimwona amepitwa na wakati, mashabiki wa West Ham nao wakasema wazi Moyes hakuwa mtu wa kuchukua nafasi ya Bilic hata kidogo na kwenye orodha katika kura zilizopigwa hapa mjini Moyes alitupwa mbali kabisa.

Kwa yeyote aliyewatazama Sunderland mara kwa mara uwanjani msimu uliopita kabla ya kushushwa daraja anaweza kusamehewa kabisa akijiuliza iwapo West Ham walifanya kazi yao ipasavyo, au walau kidogo, kabla ya kumteua Moyes kuchukua nafasi ya Bilic.

Sunderland walikuwa wakifungwa mabao ya hovyo, ambayo watu huita kama ya ‘watoto wadogo wa shule’, huku wachezaji wakiwa wamepoteza imani na Moyes aliyekuwa akiangalia tu, macho kuwa mekundu, akakuna kichwa lakini wakaendelea kufungwa tu. Hakuwa na mbinu ya kuzuia hayo.

Alikuwa hivyo tangu akiwa Manchester United alipopewa ‘zigo’ la kuvaa viatu vya Sir Alex Ferguson, akaishindwa kazi na kufukuzwa hata kabla ya miezi 12 kufika, akapumzika kidogo akatimkia Hispania akawapata Real Sociedad waliotamba wanafundishwa na aliyekuwa kocha wa Man United. Wakapigwa balaa, akaondoka 2015 na mwaka uliofuata akajiunga Sunderland na sasa West Ham.

Sikushangaa nilipoona mashabiki wa West Ham wakisikitika kupata kocha mpya, wakasema ikiwa ndiye huyu, basi sasa ni ‘RIP (Rest In Peace) West Ham’ – kifo kipo njiani. Sunderland walishinda mechi sita tu Ligi Kuu na hakuna hata moja nyumbani baada ya Desemba na Moyes aka ‘sign off’ klabu ikiwa na uwiano wa hasi mabao 40, yaani mabao waliyofungwa kwenye ligi yalikuwa 40 zaidi ya waliyofunga. Mtu wa hivyo ataweza kufanya nini West Ham? Tusubiri tuone hatima ya klabu Ligi Kuu mwakani.