Wanasiasa maarufu na klabu wanazoshangilia Ulaya

WANASIASA wengi wamekuwa bize sana kwenye maisha yao wakijaribu kufanya yale yanayowafurahisha wananchi wao ambao kwa namna moja au nyingine wamechangia kwenye kukubalika kwao.

Lakini kwa wingi wao huohuo, kuna baadhi yao wamekuwa wakipanga ratiba zao vizuri na kushiriki kwenye mambo mengine yanayohusu mpira na kuonyesha mapenzi ya timu wanazozishabikia. Hii hapa orodha ya wanasiasa mashuhuri duniani na klabu wanazoshangilia kwenye mchezo wa soka.

George Weah -

Juventus

Mwanasoka bora wa zamani wa dunia, George Weah kwa sasa ni rais wa 25 wa Liberia. Enzi za uchezaji wake, Weah anakumbukwa zaidi kwa kipindi chake bora alipokuwa kwenye kikosi cha AC Milan, lakini kitu cha kushangaza fowadi huyo wa zamani alidai siku zote amekuwa akiishabikia Juventus.

Weah alisema Juventus ilikuwa timu yake aliyokuwa akiishangilia tangu utotoni mwake na alikuwa akivaa jezi za timu hiyo katika mechi zake za utotoni na kubwa ilikuwa sababu ya Michel Platini.

Paul Kagame -Arsenal

Rais wa Rwanda, Paul Kagame ni shabiki mnazi wa timu ya soka ya Arsenal inayoshiriki mikikimikiki ya Ligi Kuu England.

Kuthibitisha mapenzi yake kwa timu hiyo, Rwanda imeamua hata kuweka udhamini wake katika jezi zinazovaliwa na wababe hao wa Emirates. Mapenzi ya Kagame kwa timu ya Arsenal hayana kificho na ndiyo maana ametoa udhamini huo muhimu, ambapo kwenye jezi za Arsenal mikononi, kuna tangazo linalosema ‘Visit Rwanda’.

Vladimir Putin – Zenit

Rais wa Russia, Vladimir Putin ni mtu wa soka na katika maisha yake imefichuka ni shabiki mkubwa wa klabu ya Zenit St Petersburg.

Mwanasiasa huyo mkubwa kabisa huko Russia, ambaye mwaka huu nchi yake iliandaa fainali za Kombe la Dunia amekuwa shabiki mkubwa wa Zenit na amekuwa akiisapoti timu hiyo waziwazi kabisa.

Queen Elizabeth II - West Ham

Baada ya kuwa siri kwa muda mrefu, watu wakiwa hawafahamu timu anayoshabiki, hatimaye Malkia wa Uingereza mwaka 2009 alifichua timu yake anayoshabikia kuwa ni West Ham United.

Siku zote alihitaji kutojionyesha kuwa na timu, lakini amebainisha mapenzi yake kwa timu hiyo yalikuwa kati ya miaka ya sitini na sabini, wakati Ron Greenwood alipokuwa kwenye timu hiyo. Malkia pia alifichua kuwa ana mapenzi na timu ya Arsenal.

Angela Merkel - Dortmund

Angela Merkel alikuwa mtu mwenye furaha kubwa wakati Ujerumani ilipobeba ubingwa wa Kombe la Dunia 2014 huko Brazil, lakini kwa soka la klabu, kansela huyo wa Ujerumani ni shabiki kwelikweli wa Borussia Dortmund. Merkel alifunga safari hadi Wembley kutazama fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya wakati ilipokutanisha timu mbili za Ujerumani, Bayern Munich na Borussia Dortmund mwaka 2013.

David Cameron - Aston Villa

Aston Villa imekuwa timu yenye bahati ya kushabikiwa na watu mashuhuru na maarufu na miongoni mwao ni Prince William na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron? Mwanasiasa huyo maarufu alizaliwa na kukulia Kusini Kaskazini mwa England, lakini apokuwa na umri wa miaka 13, Villa Park ikawa maskani yake, ambapo alichukuliwa na anko wake, Sir William Dugdale, aliyekuwa mwenyekiti wa timu hiyo. Tangu wakati huo, Cameron ni shabiki wa Aston Villa.

Barack Obama - West Ham

Aliyekuwa Rais wa Marekani, Barack Obama amefichuliwa kuwa ni shabiki mkubwa wa timu ya West Ham United inayoshiriki Ligi Kuu England. Kwa maana hiyo, Obama alikuwa kwenye wakati mgumu kwelikweli wikiendi hii baada ya juzi Jumapili timu yake anayoshabikia kuchapwa 4-0 na Liverpool katika mchezo wa kwanza wa ligi uliofanyika Anfield.

Francois

Hollande -

AS Monaco

Mwanasiasa wa Ufaransa, Francois Hollande, ambaye aliwahi kuwa rais wa nchi hiyo, alizaliwa Rouen, lakini ameripotiwa kuwa na ushabiki mkubwa na AS Monaco. Lakini, kuna kipindi aliulizwa kuhusu timu anayoshabikia, Hollande alidai anaishabikia timu ya kwao alikozaliwa na kugoma kuitaja Monaco.

Mariano Rajoy - Real Madrid

Mariano Rajoy amekuwa Waziri Mkuu wa Hispania mwaka 2011. Licha ya kuzaliwa na kukulia Galicia, Rajoy amekuwa maarufu zaidi na akifahamika kama shabiki wa Real Madrid.

Kwa kifupi tu wakati anakuwa waziri, gazeti maarufu la michezo la Hispania, AS lilifichua Rajoy amekuwa mjumbe wa Los Blancos kwa miaka 25.