MAONI: Wachezaji wenye majeraha wazingatie matibabu kamili

Muktasari:

Wachezaji wengi waliosajiliwa katika dirisha kubwa, walikumbwa na hali ya sintofahamu baada ya kuumia katika mechi za mwanzo tu wa msimu. Wapo pia waliondelea na timu zao ambao wameumia na kushindwa kutumika vilivyo msimu huu.

MSIMU huu wa Ligi Kuu Bara umekuwa na changamoto kubwa kwa wachezaji, kwani wengi wamekumbwa na majeraha katika mechi za mwanzo tu jambo ambalo linawaweka katika wakati mgumu.

Wachezaji wengi waliosajiliwa katika dirisha kubwa, walikumbwa na hali ya sintofahamu baada ya kuumia katika mechi za mwanzo tu wa msimu. Wapo pia waliondelea na timu zao ambao wameumia na kushindwa kutumika vilivyo msimu huu.

Kwa klabu ya Yanga, wapo wachezaji kama Baruan Akilimali, Amissi Tambwe, Donald Ngoma, Thaban Kamusoko na wengineo ambao wameanza msimu huu vibaya kwa kuumia na kukosa mechi nyingi.

Kwa upande wa Simba, nyota wao kama Said Mohammed ‘Nduda’, Salim Mbonde, Shomary Kapombe, Emmanuel Okwi na wengineo pia wamekuwa na majeraha ambayo yamewanyima fursa ya kutumika katika baadhi ya michezo, kama siyo yote.

Hali hiyo imekwenda hadi Azam FC ambapo nyota wake kama Shaaban Iddi, Joseph Kimwaga na wengineo wamekumbwa na majeraha ambayo yamewanyima fursa ya kucheza mpaka sasa.

Hali ya majeraha imekuwa katika timu nyingi, licha ya kwamba siyo wote wanaofahamika.

Mfano kwenye klabu ya Singida United, beki wao wa kati, Elisha Muroiwa naye alikumbwa na majeraha katika mechi za mwanzo na kushindwa kuitumikia timu yake hiyo mpya.

Ni wazi kwamba, wimbi la majeraha limekuwa kubwa katika timu nyingi, hilo likichagizwa na ugumu wa ligi pamoja na maandalizi duni kwa baadhi ya wachezaji.

Pia, ikumbukwe kuwa soka ni mchezo wa kugongana hivyo majeraha hayaepukiki kabisa. Kiwango cha kuumia tu huwa kinatofautiana kwa timu na timu lakini lazima tu wachezaji wataumia .

Pigo kubwa kwa wachezaji wa Tanzania limekwenda kwa nyota muhimu wa kikosi cha timu ya Taifa kama Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu ambao wamefanyiwa upasuaji wa goti na watakuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu.

Ulimwengu ndiye alikuwa wa kwanza kufanyiwa upasuaji wa mguu kule nchini Afrika Kusini, ambapo majeraha hayo yanamuweka nje kwa msimu mzima.

Samatta alifanyiwa upasuaji mapema mwezi huu na atakuwa nje hadi Januari, hiyo ni kwa mujibu wa madaktari wa klabu yake ya KRC Genk.

Ni wazi kwamba majeraha haya ni pigo kwa wachezaji pamoja na timu zao, jambo ambalo linawapa mawazo.

Kutokana na presha kubwa katika timu, baadhi ya wachezaji wamekuwa wakitaka kulazimisha kurejea uwanjani kabla ya wakati jambo ambalo linaweka afya zao rehani.

Tunafahamu kwamba hofu ya kuachwa na timu zao imekuwa ikiwafanya wachezaji kucheza na maumivu hivyo kukuza majeraha yao ambayo pengine yangepona kwa wakati endapo tu wangefuata maelekezo.

Wachezaji wamekuwa wakitumia dawa za kutuliza maumivu ama kufunga maeneo yanayouma ili kuweza kucheza, ikiwa ni harakati za kupambana ili wasiachwe.

Unaweza kuona presha kubwa iliyowekwa kwa beki wa Simba, Kapombe ambaye uongozi wa timu hiyo unadai kwamba amepona, wakati mwenyewe akisisitiza kuwa bado hayuko fiti.

Kapombe tayari amerejea Afrika Kusini kwenda kufanyiwa matibabu tena ili kupata uhakika wa afya yake kabla ya kuanza kucheza.

Presha ambayo imemkuta Kapombe huwa inawakuta wachezaji wengi, na wale wasiokuwa na msimamo huanza kucheza wakati wakiwa na maumivu.

Madaktari wa timu za Ligi Kuu na wengine wanaowatibia wachezaji wamekuwa wakilalamika kuwa nyota wengi hucheza kabla ya kupona kabisa.

Baadhi ya majeraha kwa wachezaji yaliongezeka na kuwa makubwa zaidi kutokana tu na kukaidi maelekezo hayo ya madaktari.

Tunapenda kuwahimiza wachezaji wa timu za Ligi Kuu na timu nyingine, kufuata maelekezo ya kiafya wanayopewa na madaktari, ili waweze kupona kwa wakati.

Si jambo jema hata kidogo kwa mchezaji kulazimisha kurejea uwanjani kabla ya kupona, hilo linaweka afya zao katika wakati mgumu.