MAONI: Wachezaji wa Zanzibar wapewe nafasi Taifa Stars

Muktasari:

Pamoja na ushindi huo, Zanzibar ilicheza soka safi na la kuvutia, ikitawala mchezo mwanzo mwisho na kufanya mashambulizi mengi zaidi ya Stars.

ZANZIBAR imezidi kuthibitisha ina wachezaji bora na wa viwango vya juu, baada ya juzi Alhamisi kuifunga Kilimanjaro Stars mabao 2-1 katika michuano ya Kombe la Chalenji inayoendelea nchini Kenya.

Pamoja na ushindi huo, Zanzibar ilicheza soka safi na la kuvutia, ikitawala mchezo mwanzo mwisho na kufanya mashambulizi mengi zaidi ya Stars.

Kwa kifupi Zanzibar ilistahili kushinda mchezo huo kwani iliizidi mbali kiwango Kilimanjaro Stars.

Katika hali ya kawaida, Killi Stars ilipewa nafasi kubwa ya kushinda mchezo huo kutokana na kuwa na wachezaji wengi wanaounda Taifa Stars na wanaotamba katika timu mbalimbali za Ligi Kuu Bara.

Mambo yalikwenda tofauti na Kill walijikuta wakiomba mpira umalizike mapema, kutokana na soka safi lililotandazwa na vijana hao kutoka upande wa pili wa Tanzania.

Ni wazi sasa, Zanzibar wameendelea kuthibitisha wana wachezaji wazuri na wenye sifa ya kuwa katika kikosi cha Taifa Stars ambacho hubeba sura ya Jamhuri ya Muungano katika mashindano ya kimataifa.

Ajabu ni kwamba kikosi cha Zanzibar kilichoshinda juzi kina wachezaji wawili tu katika timu yetu ya Taifa. Wachezaji hao ni Mudathir Yahya pamoja na Mohammed Issa ‘Banka’.

Jambo la kushangaza zaidi, Mudathir pekee ndiye mchezaji wa Zanzibar anayeanza katika kikosi cha Stars. Wachezaji wengi wa Zanzibar wamekuwa wakiachwa katika timu ya taifa kwa madai ligi yao ni dhaifu. Hali inajionyesha sasa kuwa pamoja na yote, wachezaji wa Zanzibar bado wana viwango vya juu na wanatakiwa kupewa nafasi katika timu ya Taifa.

Ilifikia hatua makocha wa Taifa Stars waliita vikosi vyao bila kujumuisha mchezaji yeyote wa Zanzibar, jambo ambalo liliacha maswali mengi kama ni kweli viwango vya nyota hao vimeporomoka kiasi hicho. Sasa mambo yamekuwa hadharani na itashangaza kuona kikosi cha Taifa Stars kinatajwa bila kuwa na nyota wa Zanzibar.

Japokuwa hatuwezi kuwataja kwa majina, tunaamini kwamba makocha wa timu ya Taifa, Salum Mayanga na Novatus Fulgence wameona ubora wa vijana wa Zanzibar na wataanza kuwafuatilia zaidi ili wawape nafasi katika timu yao.

Katika upande mwingine, kipigo kutoka kwa Zanzibar kinapaswa kuiamsha Kilimanjaro Stars na kutuma jumbe kwamba nyota wake wameshuka viwango na wanatakiwa kujituma zaidi.

Kwanza, viwango vya washambuliaji wa Stars viko chini, kwani timu hiyo imecheza dakika 180 na kufunga bao moja tu. Nyota wake Elias Maguli, Yahya Zayd na Danny Lyanga wanapaswa kujirekebisha na kupambana ili kufuta makosa yao.

Ni tofauti na Zanzibar ambayo katika mechi mbili zilizopita imefunga mabao matano, ikiwemo matatu iliyowafunga Rwanda kwenye mchezo wa ufunguzi.

Pili, viwango vya wachezaji wa nafasi ya ulinzi ni vya kawaida na wengine vinatia mashaka, hasa ikitazamwa kuwa mabao yote Stars iliyoruhusu mbele ya Zanzibar yalitokana na uzembe uliotokea katika beki ya kulia. Ule moyo wa upambanaji pia katika timu yetu umeshuka, tofauti na kipindi cha nyuma wachezaji walijituma vilivyo ili kuhakikisha tunapata ushindi.

Tunapenda kuliomba benchi la ufundi la Kilimanjaro Stars kwa kushirikiana na lile la Taifa Stars, kufanya uchunguzi wa mambo yanayoishusha morali timu yetu ya Taifa, ili iweze kwenda katika mwelekeo sahihi. Wachezaji pia wajitafakari, kwani kufungwa na timu ndogo kama Zanzibar ambayo ilikwenda Kenya kwa usafiri wa basi ni aibu isiyofutika haraka.

Wachezaji wa Kilimanjaro Stars wanaishi maisha bora zaidi ya wenzao wa Zanzibar lakini sasa matokeo yake uwanjani viwango vinakuwa tofauti na wenye maisha mazuri wanazidiwa tena.

Katika upande mwingine, nafasi ya Kilimanjaro Stars kusonga mbele katika mashindano hayo ni finyu, na inahitajika nguvu ya ziada kushinda mechi mbili zijazo dhidi ya wenyeji Kenya na wapinzani wengine wabishi, Rwanda.

Stars inatakiwa kuthibitisha ubora wake dhidi ya Kenya kwa kupata ushindi, ambao utawaweka wenyeji hao katika wakati mgumu wa kufuzu, vinginevyo safari itakuwa imeishia hapo.

Benchi la ufundi linatakiwa kuwa na mbinu mbadala ili kushinda mechi hizo ngumu ambazo ziko mbele yetu.