Waafrika watakaosimama kati Russia

Tuesday June 12 2018

 

IIKIWA imesalia siku moja tu kabla ya ufunguzi wa fainali za Kombe la Dunia zinayofanyika kule Moscow, Russia, timu zote 32 zinazoshiriki zimeshawasili na sasa kinachosubiriwa ni kupulizwa tu kipenga kazi ianze.

Timu zimewasili, mashabiki nao wanazidi kumiminika, lakini bila kuwasahau waamuzi ambao ndio muhimu zaidi kuwepo kuamua nini kifanyike ndani ya uwanja.

Waamuzi hao ni 36 wa kati pamoja na wasaidizi wao 63 isipokuwa wawili tu, Mkenya Aden Marwa na mwingine raia wa Ghana ambao wameondolewa kutokana na tuhuma za rushwa. Hata hivyo, wengine watasimamia kipute hicho kinachorajiwa kufikia tamati Julai 15, mwaka huu.

Ijapokuwa marefa hao wawili kutoka Afrika tayari wameshaondolewa, bado bara hili litawakilishwa na marefa sita wa kati. Ni jambo la kufurahisha kwa kuwa na makocha kwenye dimba hilo, hasa ukizingatia kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 80, michuano hiyo haitakuwa na refa hata mmoja kutoka Uingereza.

Mwanaspoti linakuletea marefa sita Waafrika watakaopuliza kipyenga pale Russia.

MEHDI ABID CHAREF, Algeria

UMRI: Miaka 37

Amekuwa refa katika Ligi Kuu ya Algeria tangu mwaka 2005. Beji ya Fifa aliipata mwaka 2011 na anatajwa kuwa mmoja kati ya marefa bora kutoka Afrika. Charef amechezesha mechi kadhaa kubwa za kimataifa zikiwamo za michuano ya CAF U20 Championships, pamoja na ile ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON). Hivyo, kutokana na uwezo wake, mwaka huu alikuwa miongoni mwa marefa walioteuliwa kuwania tuzo ya ya refa bora wa CAF.

MALANG DIEDHIOU, Senegal

UMRI: Miaka 45

Huyu sio kati tu, hata kwenye kompyuta ni mtaalamu. Raia huyu wa Senegal alitumika sana kwenye michuano ya AFCON 2015. Kwenye michuano ya 2017 Confederations Cup iliyofanyika Russia, alitumika kama refa wa video (VAR-Video Assistant Refree). Pia, alichezesha mechi mbili za Olimpiki ana kila sababu za kufuzu kwa Kombe la Dunia.

Mwaka huu alikuwa miongoni mwa marefa waliowania tuzo ya mwamuzi bora wa CAF. Hata hivyo, kipengele hicho kiliondolewa huku Rais wa CAF, Ahmed Ahmed akisema waliamua kufutilia mbali kipengele hicho ili kutotengeneza mazingira ya kiufisadi kwenye tasnia ya uamuzi.

BAKARY PAPA GASSAMA, Gambia

UMRI: Miaka 39

Alipata beji ya Fifa mwaka 2007 na mpaka sasa amechezesha mechi 74 katika mashindano 15 mbalimbali ikiwemo Kombe la Dunia.

Ndiye refa wa pekee kutoka Afrika aliyetumika kama mwamuzi wa kati kwenye mashindano ya Cofederations Cup 2017 akitumika kwenye mechi moja ya Kundi A iliyowakutanisha Mexico na New Zealand huku Aden Marwa akiwa mmoja wa wasaidizi wake.

Mara tatu Bakary alitawazwa kuwa refa bora wa Bara Afrika 2014, 2015, 2016, kipengele ambacho sasa kimefutiliwa mbali. Aliwahi pia kutumika kwenye mechi za Olimpiki 2012 akiwa kama mwamuzi wa nne.

Ndiye refa aliyechezesha mechi ya Kundi B kati ya Uholanzi na Chile kwenye Kombe la Dunia 2014 kule Brazil. Mwaka mmoja baadaye akachezesha fainali ya AFCON kati ya Ghana na Ivory Coast.

GEHAD GRISHA, Misri

UMRI: Miaka 42

Aliongezwa kwenye orodha ya marefa wa Fifa mwaka 2008. Kachezesha AFCON 2014 na 2015. Vile vile alitumika kwenye mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia. Mwaka huu alikuwemo pia kwenye orodha ya marefa waliotakiwa kuwania tuzo ya mwamuzi bora.

JANNY SIKAZWE, Zambia

UMRI: Miaka 39

Ndiye aliyechezesha fainali ya Klabu Bingwa ya Dunia mwaka 2016 kule Japan. Pia, ndiye refa aliyesimamia fainali ya AFCON 2017. Kwa jumla kahusishwa kwenye michuano mitatu ya AFCON. Sikazwe ameshiriki kwenye michuano 12 akichezesha mechi 58 ikiwemo Kombe la Dunia 2015 U15 na ile ya U20 ya mwaka 2018.

WEYESA BAMLAK TESSEMA, Ethiopia

UMRI: Miaka 38

Alipewa beji ya Fifa mwaka 2009. Kahusishwa sana kwenye mechi za CAF. Kwa jumla kahusika katika mashindano saba yanayotambuliwa na Fifa. Mbali na kazi ya urefa, Tessema ni daktari.