Tusiilaumu TFF tu, tatizo klabu zetu

Muktasari:

  • Inawezekana ni ngumu kuzikwepa klabu hizo mbili kubwa nchini, ndivyo ilivyo. Hizi ni klabu za urithi ambazo watu wanazaliwa ndani ya jamii na kukuta wazazi wao wana utamaduni wa kuzishabiki klabu hizo na kufuata mkondo huo. Haishangazi kusikia kiongozi wa Kagera Sugar akija kupiga kura katika Uchaguzi wa Simba ama Bosi wa Toto African kushiriki Uchaguzi wa Yanga.

SIASA za soka la Tanzania zinashangaza sana. Zimejaa fitina na ujanja ujanja. Kila jambo katika soka letu limekuwa likipimwa kwa itikadi za Usimba na Uyanga tu.

Kuanzia timu ya taifa mpaka hadi utendaji wa viongozi wanaosimamia soka hilo. Jambo lolote linalotokea kwenye soka letu, kipimo kikuu ni Usimba na Uyanga, hata kama wakati mwingine hutokea kwa bahati mbaya bila kuwepo kusudio.

Inawezekana ni ngumu kuzikwepa klabu hizo mbili kubwa nchini, ndivyo ilivyo. Hizi ni klabu za urithi ambazo watu wanazaliwa ndani ya jamii na kukuta wazazi wao wana utamaduni wa kuzishabiki klabu hizo na kufuata mkondo huo. Haishangazi kusikia kiongozi wa Kagera Sugar akija kupiga kura katika Uchaguzi wa Simba ama Bosi wa Toto African kushiriki Uchaguzi wa Yanga.

Hata viongozi wanaoingia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wakati mwingine hupenya kwa kura zinazolalia katika mirengo ya klabu hiyo. Ndio maana unaweza kumsikia kiongozi wa Simba akidai kuwa, eti utawala wa Jamal Malinzi uliibania Simba. Ukiuliza kivipi, huwezi kupata jibu la moja kwa moja zaidi ya hisia za kishabiki.

Leo hii, utasikia kelele za upande wa Yanga kwamba TFF imejaa Usimba kwa vile tu kuanzia Rais wake, Katibu Mkuu mpaka Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB) na baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ni watu wenye mrengo wa Msimbazi. Hata hivyo ukiuliza sababu ya kuona waliopo madakarani wanaliongoza TFF kwa ushabiki, hupati majibu yoyote ya kuthibitisha hilo.

Wengi wamekuwa wakiongozwa na hisia tu wakiamini kila linalofanyika Karume, yalipo makao makuu ya TFF yanatokana na Usimba au Uyanga wa viongozi wa shirikisho hilo la soka, lakini kiuhalisia hakuna kitu kama hicho.

Juzi kati tu, kwenye mitandao ya kijamii na hata baadhi ya redio na magazeti yaliibuka hoja juu ya mechi 11 mfululizo za Yanga zitakazochezwa jijini Dar es Salaam.

Hoja ni zile zile kwamba mechi hizo zimepangwa kimkakati kuisaidia Yanga, huku wengine wakidai ni mtego kwa Vijana wa Jangwani, kwani itakuja kuipa faida Simba mwishoni mwa msimu wakati itakapofululiza nazo kucheza Dar. Yale yale ya Kulwa na Dotto. Mmoja akibebwa, mwingine lazima alie. Ratiba inayopigiwa kelele leo ndio itakayokuja kushangiliwa kesho na watu wa Simba. Kwa sababu Simba nayo lazima itacheza mechi zake Dar es Salaam hata kama itakuwa ugenini.

Wengine wamediriki kuinyooshea vidole TFF na Bodi (TPLB) kwamba imefanya makosa makubwa kuipangia Yanga ratiba ya namna hiyo. Wanaamini ni ajenda ya siri iliyozibwa na unazi wa viongozi wanaoiongoza TFF na TPLB. Lakini wakati wanatoa lawama hizo wanasahau kuwa, tatizo wala sio TFF/TPLB bali ni klabu zenyewe na kama wangeipitia vyema ratiba hiyo wangebaini walistahili kutoa pongezi kwani itaziokoa baadhi ya klabu katika suala la kiuchumi.

Kadhalika ni lazima timu zote 20, zicheze mechi 19 nyumbani na nyingine kama hizo ugenini, iwe sasa ama baadaye, lakini lazima zitacheza mechi hizo.

Ifahamike wazi Ligi Kuu haina Mdhamini Mkuu kwa sasa na kanuni zinaeleza wazi, timu wenyeji ndio wanaochukua mapato yote ya mlangoni katika mechi za ligi hiyo msimu huu. Ukifuatilia ratiba hiyo, katika mechi hizo 11, inaonyesha ni mechi saba tu Yanga ndio watakuwa wenyeji kuanzia leo Jumapili dhidi ya Stand United, kisha Coastal Union, Singida United, Mbao, Alliance FC, Lipuli na Ndanda FC.

Mechi zao nyingine nne ambazo Yanga itacheza jijini Dar es Salaam ni dhidi ya JKT Tanzania, Simba, KMC na African Lyon, ila wakihesabika kuwa wapo ugenini.

Kila shabiki anafahamu kuwa, Dar es Salaam ndio Mkoa wenye timu nyingi katika Ligi Kuu. Una klabu sita zikiwamo Simba, Yanga, Azam, KMC, African Lyon na JKT Tanzania, pia kuna baadhi ya mechi kwa ukubwa wa klabu hizo hulazimishwa kupigwa jijini Dar ama viwanja vyenye uwezo wa kumudu wingi wa mashabiki.

Yanga na Simba hazichezi Manungu, Turiani dhidi ya Mtibwa Sugar badala yake wanapelekwa Jamhuri, Morogoro. Pia haziendi Mabatini, Mlandizi kuvaana na Ruvu Shooting na badala yake mechi zao huamishiwa Taifa ama Uhuru.

Pia klabu hizo hazipelekwi Mwadui Complex kuvaana na Mwadui na badala yake mechi zao huchezwa Kambarage, Shinyanga. Ni juzi tu ndio wamelazimishwa kwenda Azam Complex, Chamazi kuvaana na Azam, lakini kabla ya hapo hata mechi zao zilizuiwa kuchezwa huko, kisa mashabiki lukuki walionao.

Sawa huu ni ujinga tu uliibuliwa kwa kuzifanya Yanga na Simba kuwa maalum, lakini utamaduni huu umeanzishwa na kuzoeshwa na mabosi wa soka nchini pamoja na klabu hizo kubwa na hata wale wanaoziongoza nyingine katika kuhakikisha wanavuna fedha za kutosha dhidi ya watani hao wa jadi.

Kadhalika klabu nyingi zikiwamo Simba na Yanga hazina viwanja vyao wenyewe, hivyo zinapokuwa na mechi, hulazimika kucheza Uwanja wa Taifa ama Uhuru kunakoonekana kuwa ni faida kwa klabu kubwa.

Zinapocheza Simba na Yanga huwezi kuona tofauti yoyote ya timu mwenyeji ama mgeni, labda kwenye ishu za mapato tu. Kwa kuwa klabu hizo hazina viwanja vyao badala yake kutegemea viwanja vya serikali tu.

Hapo utailaumu vipi TFF? Ukiondoa Azam waliojenga uwanja wa kisasa, klabu nyingine zenye kumiliki viwanja, bado viwanja vyao havikithi haja na uwezo wa kumudu idadi kubwa ya mashabiki kwa kuwa havina miundo mbinu salama kwa watamazaji. TFF hapo inahusika vipi kutengeneza mipango ya kuzibeba Simba ama Yanga?

JKT Tanzania ina uwanja wao kule Mbweni, lakini jinsi ulivyojengwa hauwezi kuruhusu Simba na Yanga kwenda kucheza kule ni kama ilivyo kwa Mabatini ama Manungu.

Lakini kuna wakati wadau wanasahau kuwa kuhamishwa kwa mechi hizo dhidi ya Simba na Yanga kwenye viwanja vyenye uwezo wa kubeba watu wengi ni faida kwa timu wenyeji. Mtibwa wanaweza kuvuna fedha nyingi wakicheza Jamhuri, kuliko wangetaka mechi zao zichezwe Manungu.

Ni sawa na JKT, Ruvu Shooting na hata Mwadui. Katika zama hizi za matumizi ya kanuni za timu mwenyeji kuvuna fedha zote, unaweza kuona ni faida kwa klabu zitakazozifuata Yanga na Simba jijini Dar es Salaam, maadam wao ndio wanaokuwa wenyeji.

Ndio maana tunasema wakati tunailaumu TFF na TPLB kwa ratiba inayoonekana kama ya kimagumashi, pia iangaliwe upande wa pili wa shilingi na kuchungulia faida inazopata klabu katika zama hizi za Ligi Kuu kuendeshwa bila mdhamini.

Vile vile wanaopiga kelele leo ndio hao hao watakaokuja kushangilia pale Simba itakaporudi kukamilisha ratiba ya kucheza mechi mfululizo jijini Dar hata kama baadhi ya mechi itakuwa wageni, huku wale wa Yanga nao wakiishia kulalama.

Wanaolalama sasa wanataka Yanga ikacheze na Lyon Tanga? Wanataka Simba ikacheze na KMC Mtwara ama Tabora? Kupelekwa mechi mikoani sio tatizo, lakini ndivyo viwanja walivyoviainisha kwenye leseni zao wakati wakijisajili kwa Ligi Kuu msimu huu? Hapo ndipo ninapokumbusha kuwa, tatizo halipo TFF tu, bali hata kwa klabu zetu na bahati mbaya Usimba na Uyanga umetutia upofu kiasi cha kushindwa kuona ukweli ulivyo!