Tunaruhusiwa kuanza kuota ndoto ya kwenda Cameroon

Muktasari:

  • Ilikuwa suluhu ya ajabu. Ilikuwa mechi ya pili katika utawala wa kocha, Marcio Maximo. Mechi ya kwanza Stars walishinda 2-1 pale Uwanja wa Taifa dhidi ya Burkina Faso. Mechi ya pili ndio hii ilikuwa dhidi ya Msumbiji. Mwanga ulionekana, ila ukaja kuharibika dakika za mwisho.

ALIANZISHA ndoto Nadir Haroub ‘Cannavaro’ katika hoteli moja pale Maputo Oktoba 2006. Baada ya kutoka suluhu ya bila kufungana na Msumbiji, Cannavaro akawasha moto wa kuongea ovyo kwa wenzake kwamba sare hiyo ilikuwa inamaanisha kuwa Taifa Stars walikuwa wanakwenda Afcon Ghana mwaka 2008.

Ilikuwa suluhu ya ajabu. Ilikuwa mechi ya pili katika utawala wa kocha, Marcio Maximo. Mechi ya kwanza Stars walishinda 2-1 pale Uwanja wa Taifa dhidi ya Burkina Faso. Mechi ya pili ndio hii ilikuwa dhidi ya Msumbiji. Mwanga ulionekana, ila ukaja kuharibika dakika za mwisho.

Miaka 12 baadae nadhani tunaruhusiwa kuiota ndoto hii tena. Hesabu za vidoleni zinaonyesha tuna kila sababu ya kuanza kuota ndoto hii na kujaribu kuitimiza kama tutaamua kusafiri pamoja katika ndoto hii ya kusisimua. Tunaweza kwenda Cameroon mwakani tukiwa makini hasa kama tulijifunza tulivyoikosa nafasi ya kwenda Ghana, 2008.

Mechi ya kwanza tuliharibu pale Chamazi. Wakati mwingine unashangaa, kwanini TFF waliamua kuipeleka mechi katika uwanja ambao sehemu ya kuchezea ni ndogo. Walesotho wakaubana uwanja wakatoka sare ya bao 1-1.

Kama tungecheza na Lesotho katika uwanja mpana kama ule, akina Mbwana Samatta wangepata nafasi nzuri ya kuwakimbiza Lesotho na kupata matokeo. Hata hivyo sio mbaya. Tunawadai pointi tatu katika uwanja wa kwao. Ni kitu ambacho kinawezekana.

Mechi ngumu zaidi kwa Stars ugenini ilikuwa dhidi ya Uganda ugenini. Kama tumechukua pointi moja dhidi ya ugenini Kampala huku Lesotho na Cape Verde wakitoka sare pale Maseru basi kuna uwezekano mkubwa wa Stars kwenda Afcon pale nyumbani kwa kina Samuel Eto’o mwakani kama tukipiga hesabu zote vizuri.

Kitu cha msingi kwa Stars ni kuhakikisha walau tunaambulia pointi nyingine moja ya ugenini dhidi ya Cape Verde na kisha kushinda katika mechi ya marudiano. Halafu hapo hapo kuna mambo mawili tunaweza kufanya. kwanza ni kumuombea Mganda awe mbabe wa kundi. Ashinde mechi zake mbili dhidi ya Lesotho na ajishindilie kileleni.

Kama atashinda na Cape Verde na kujihakikishia nafasi bado haina ubaya. Zinahitajika timu mbili katika kila kundi kama unapata mbabe mmoja sio mbaya kwa sababu anakusaidia kuwazamisha watu ambao wangeweza kuwania nafasi ya pili na wewe. Wakati huo huo huku Stars nao wakifanya kazi yao. Mwisho wa siku, pambano la mwisho la Stars litakuwa dhidi ya Uganda katika Uwanja wa Taifa kama tumefanya kazi yetu vizuri huku Uganda akiwa ameshapita, basi inaweza kuwa mechi rahisi. Lakini kwanza tunapaswa kuifanya kazi yetu.

Kitu cha msingi kwa sasa ni kushikamana. Kurudisha ari na uzalendo katika timu. Wakati ule tukijaribu kuisukuma timu kwenda Ghana katika Afcon ya 2008 hatukuwa na wachezaji wa kulipwa wanaocheza nje ya mipaka yetu. Leo tuna wachezaji tisa ambao wanatoka nje na bahati nzuri ni kwamba wote wanafanya vizuri katika klabu zao. Kitu kizuri zaidi wanaisaidia timu. katika mechi ya Uganda walidhihirisha uwezo wao na wachezaji nane kutoka nje walitumika katika mechi hiyo.

Hatukuwahi kupata fursa hii katika siku za nyuma, lakini vile vile kundi la wachezaji hawa limetokea katika timu za taifa za vijana miaka ya karibuni. Katika kikosi kile cha Stars ambacho kilikuwa kinaota ndoto ya kwenda Ghana asilimia 98 ya wachezaji walikuwa hawajawahi kuiwakilisha Tanzania katika ngazi ya vijana. Mpira ulikuwa mgumu.

Zaidi ya kila kitu ni kwamba kocha, Emmanuel Amunike anaonekana kuwa kocha ambaye tunaweza kusafiri naye safari hii. Kama akicheza kimbinu zaidi katika mechi za ugenini kama tulivyofanya dhidi ya Uganda basi tunaweza kuchuma pointi za ugenini pia. Katika mashindano hiki ni kitu muhimu.

Tatizo kubwa ambalo linaweza kuisumbua Stars ni Usimba na Uyanga uliojaa katika vichwa vya mashabiki na viongozi wa soka nchini, hasa wale wa hizo klabu. Lilifanyika kosa la kiufundi kwa wachezaji wa Simba kushindwa kuripoti, lakini imeanza kuwa nongwa kutoka kwa mashabiki wa Simba kwenda kwa mashabiki wa Yanga au mashabiki wa Yanga kwenda kwa Simba. Haina maana.

Wachezaji wa Simba wanahitajika katika kikosi cha Stars. Wote ni muhimu. Wachezaji ambao hawaitwi nao ni muhimu kama walioitwa. Nani alijua kwamba David Mwantika angeonyesha umuhimu ule katika pambano dhidi ya Uganda?

Tatizo kubwa la Watanzania ni kuzipenda Simba na Yanga kuliko kuupenda mpira. Kama tukiamua kuupenda mpira japo kwa jicho la kuitakia mema Taifa Stars tu naamini tunaweza kwenda Cameroon. Kama hizi fitina za Simba na Yanga zikiungana kwa pamoja dhidi ya wageni wa kundi letu basi tunaweza kwenda Cameroon.