Tumewasahau kirahisi Mandawa na Mkude

Muktasari:

  • Mandawa alikuwa amevaa jezi ya BDF, timu ambayo anachezea kwa sasa. Anaonekana kutamba katika Ligi Kuu ya Botswana na sio mbaya sana kama angetangazwa na Kocha Salum Mayanga katika kikosi cha Taifa Stars ambacho kinatarajiwa kucheza na Algeria na DR Congo hivi karibuni.

KABLA hawajafika Tanzania kucheza kandanda safi dhidi ya Yanga, Township Rollers walikuwa na wakati mgumu wa kumkaba mshambuliaji mahiri wa kimataifa wa Tanzania, Rashid Mandawa. Aliwapiga hat trick katika pambano gumu pale Gaborone.

Mandawa alikuwa amevaa jezi ya BDF, timu ambayo anachezea kwa sasa. Anaonekana kutamba katika Ligi Kuu ya Botswana na sio mbaya sana kama angetangazwa na Kocha Salum Mayanga katika kikosi cha Taifa Stars ambacho kinatarajiwa kucheza na Algeria na DR Congo hivi karibuni.

Baada ya kiwango cha Rollers dhidi ya Yanga inapaswa tuanze kuiheshimu Ligi Kuu ya Botswana taratibu. Wanaonekana wanakuja vizuri. Tuache kukariri. Kama Mandawa ni mmoja kati ya wafungaji bora wa ligi hiyo, kwa nini asiitwe?

Sio anaitwa kwa ajili ya kuwa mshambuliaji wa kudumu, hapana, anaitwa kwa sababu ya kuangalia kama amebadilika kwa kiasi kikubwa kuanzia pale alipoishia wakati anacheza soka la Tanzania. Pia anaitwa kwa sababu hizi ni mechi za kirafiki na makocha huzitumia kwa ajili ya kupima viwango vya wachezaji.

Inatia moyo wachezaji wanaokwenda kujaribu bahati zao nje ya nchi, hasa wale ambao tulifahamu vyema viwango vyao wakati wakiwa nchini. Alikuwa kijana mwenye uwezo, umbo zuri na mpambanaji. Sijui kama TFF wanamfuatilia huko aliko lakini anaonekana anafanya vizuri.

Ninadhani kwa sasa nafasi ya Thomas Ulimwengu ingekwenda kwake. Ni rahisi tu kuamua. Thomas ambaye ni mmoja kati ya washambuliaji bora nchini hajacheza kwa muda mrefu kutokana na kuwa majeruhi. Kwa sasa ameenda kuanza upya Bosnia baada ya kupona goti lake. Anapokuwa fiti, Thomas ni mchezaji ambaye anastahili kuanza katika kikosi cha Stars. Ni mpambanaji.

Kwa sasa angeweza kumpisha mchezaji kama Mandawa wakati yeye akianza kujiweka fiti upya Bosnia. Hizi ni mechi mbili za kirafiki tu. Baada ya hapo kama Thomas akiwa fiti angeweza kurudi kikosini katika siku za usoni.

Kwa Mandawa mwenye mabao 12 Ligi Kuu ya Botswana, kama angerudi katika kikosi cha Stars ambacho amewahi kuchezea siku za nyuma, si ajabu angekuwa anajiongezea wasifu mzuri katika rekodi zake kwa klabu za Afrika Kusini ambazo hapana shaka zinaiangalia ligi hiyo kwa karibu.

Kumekuwa na ushindani mkubwa katika eneo la ushambuliaji Taifa Stars kwa sababu mastaa wengi kwa sasa wanacheza nje. Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu, Saimon Msuva (ambaye anachezeshwa kama mshambuliaji wa Jadida), Farid Mussa, Elius Maguli ambaye hana timu lakini ana rekodi ya kucheza nje.

Sio mbaya kuanza kuangalia fomu zao huko waliko ingawa wote ni wazuri. Wote tunafahamu ubora wao wakiwa fomu, lakini katika mechi za kirafiki tunapaswa kuwa makini kuwajaribu wale ambao wameshika chati.

Kwa upande mwingine kuna huyu Jonas Mkude. Sijui kwa nini Mayanga hajamchagua. Mayanga alikuwa na wakati mzuri wa kutomchagua Mkude wakati ule akiwekwa benchi na James na Kotei. Lakini sasa kocha anawatumia wote kwa pamoja na Mkude amekuwa akicheza soka maridadi la kiwango. Ni mmoja kati ya viungo mahiri, lakini ukiangalia vile vile tayari amecheza mechi kadhaa za kimataifa msimu huu akiwa na Simba. Inampa nafasi nzuri ya kucheza mechi za kimataifa za Taifa Stars kwa sasa.

Sio kwamba Mandawa na Mkude ni wachezaji wenye haki ya kuitwa katika timu ya taifa kuliko wachezaji wengine walioachwa, hapana, ni kwa sababu wana vigezo fulani tofauti kwa sasa. Zipo nyakati ambazo naweza kurudi hapa na kusema hawastahili kuitwa kwa nyakati hizo. Kwa mfano, si lazima sana kwa shabiki kulalamika kuachwa kwa Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ wa Simba kwa sababu ukweli, kwa sasa anasugua benchi mbele ya Asante Kwasi. Kama anaitwa Gadiel na kisha Tshabalala anakaa benchi unaweza kuelewa sababu.

Kama Mo Ibrahim haitwi katika kikosi cha Stars unaweza kuelewa kwa nini. Hatumwoni katika kikosi cha Simba. Unaweza kumtetea kocha. Lakini kuna wengine ambao wanafanya vizuri kiasi kocha anaweza asiwaite lakini akatupa sababu za kutowaita.

Tuanze kuipeleka timu ya Taifa kwa wachezaji mbalimbali ambao wanaonyesha uhodari wao ndani na nje ya nchi. Kama wanakidhi vigezo na wanaweza kuongeza kitu sio mbaya kuwajaribu kuliko hii ya kukariri.

Tatizo kuna wakati tunavutika zaidi na wachezaji wanaosema wanacheza England na tunajaribu kuwaita wakati pale England wanacheza katika timu za madaraja ya chini.

Vinginevyo kila la kheri kwa Mayanga. Ninadhani TFF wamekaa chini na kujiuliza kwa nini walipigwa mabao 7-0 na Algeria ugenini na sasa wanataka kujaribu kujiuliza tena. Sio uamuzi mbaya lakini wanahitaji kupambana kweli kweli. Algeria wana hasira ya kukosa kwenda Kombe la Dunia pale Russia.