MAONI YA MHARIRI: TFF msisubiri maafa ndipo mchukue hatua kwenye FDL

UPO msemo wa Kiswahili unaosema, mdharau mwiba mguu huota tende na kuna mwingine unaodai kila mficha maradhi mauti huja kumuumbua.

Mambo yanayoendelea kwenye mechi za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwa mashabiki kuanzisha vurugu dhidi ya wenzao, kuna siku yatatuletea aibu katika soka la Tanzania.

Kama Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) pamoja na Bodi ya Ligi (TPLB) sambamba na wasimamizi wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) hawataanza kuchukua tahadhari za mapema katika mechi za ligi hiyo kuna hatari ya kuja kutokea maafa.

Hii ni mara nyingine tunarudia kuitahadharisha TFF juu ya vurugu za mara kwa mara ambazo zimekuwa zikijitokeza kwenye mechi za FDL.

Vurugu na uhuni huo usiokubalika katika ulimwengu wa soka, zimekuwa zikitokea katika mechi za ligi hiyo kwa muda mrefu sasa, tangu enzi za Leodegar Tenga, yakajitokeza pia enzi za Jamal Malinzi na Utawala wa Wallace Karia umezipokea kutokana na kujitokeza ndani ya mwezi mmoja tu wa ligi hiyo.

Mwanaspoti tumekuwa tukikemea na kulaani sambamba na kuzikumbusha mamlaka na klabu husika kudhibiti vitendo hivyo vinavyoliharibia sifa ya soka la Tanzania, lakini ni kama watu wametia pamba masikioni. Mwanzoni mwa msimu vurugu kubwa zilitokea Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora katika pambano la wenyeji Rhino Rangers na Alliance Academy ya Mwanza, tukadhani ni bahati mbaya na mambo yatarekebishwa.

Hata hivyo, matukio yamekuwa yakiendelea kujiri na kuharatisha usalama wa watu wanaoenda uwanjani kuangalia soka la ligi hiyo.

Wikiendi hii iliyopita tena zimezuka vurugu kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro wakati wa mchezo kati ya wenyeji Mawenzi Market dhidi ya Mlale JKT.

Tunaamini vurugu kama hizi zinafanyika na kuzidi kukithiri pengine kwa vile hakuna usimamizi ama uangalizi mzuri katika mechi za ligi hiyo. Matukio kama haya katika FDL na hata SDL yamekuwa yakiota mizizi kwa muda mrefu, baadhi ya timu zimekuwa zikiadhibiwa kwa kutozwa faini, lakini bado hazijaweza kuleta tija yoyote.

Ingekuwa vyema kwa TFF na mamlaka zinazosimamia mechi za ligi hizo wakati jitihada katika kukomesha matukio hayo, ikiwamo viongozi wa klabu kuwapiga msasa mashabiki wao kuachana na mambo ya ovyo katika soka.

Soka ni mchezo wa kistaarabu wenye kujenga urafiki, udugu na umoja miongoni mwa wadau wake, hivyo matukio ya kupigana iwe kabla ama baada ya mechi ni ushamba ambao unatakiwa upigiwe kelele na kukemewa ili uishe.

Mambo kama hayo ndiyo yanayochangia kuwa vikwazo kwa wadau hususan wadhamini kutaka kuzidhamini ligi hizo na kufanya FDL na SDL kuendeshwa kama mechi za mabonanza ama michuano ya ndondo. Haiwezekani mechi za duru la kwanza zianze kwa vurugu, vipi kwa mechi za lala salama zinazoamua timu za kupanda daraja? Si tunaweza kushuhudia maafa kama yaliyokaribia kutokea msimu uliopita wa FDL katika mechi za Mshikamano dhidi ya wenyeji wao Lipuli? TFF isifanye mchezo na mambo ya aina hii, lazima watupie macho na kuzifuatilia kwa karibu ligi hizo za chini kama ambavyo wamekuwa makini katika mechi za Ligi Kuu Bara.

Kama tunaendelea kuwalea na kuwaacha wahuni wanaolivuruga soka letu kwa matendo yao ya ovyo, kuna siku tunaweza kushuhudia maafa kwa sababu siku zote mzaha mzaha mwisho hutumbuka usaha.

Tunadhani kuna haja ya TFF kushirikiana na hata jeshi la polisi kuweza ulinzi madhubuti na kuwanasa vinara wa vurugu kwa kuwafungulia kesi na kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria ili kutoa funzo kwa wengine.

Kutochukuliwa hatua zozote za kisheria kwa watenda uhuni huo, huenda ni sababu ya kukithiri kwa matukio hayo, kwani hakuna mwenye uoga kwa sababu wanajua klabu itatozwa faini tu na fedha zitalipwa kisha mambo yataendelea.

Tusiwanyamazie wachache wanaotaka kuvuruga soka letu, lakini pia TFF ni lazima wawe wakali na kushirikiana na klabu kuwadhibiti wahuni hao ili kufanya  wengine waingie woga, la sivyo ule msemo wa mchelea mwana kulia.... utakuja kuikumba TFF na mamlaka nyingine za kusimamia ligi hizo za chini. Tujihadhari.